Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dk.Damas Ndumbaro akieleza jambo katika
uzinduzi wa mashine ya kisasa ya kuchakata mazao ya misitu, Kulia ni
Mshauri Mkuu wa Ufundi wa FORVAC Juhan Harkonen na Kushoto ni Nette
Korhonen Mshauri Anayechipukia Wakimataifa.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk.Damas Ndumbaro
akikata utepe kuzindua mashine ya kisasa ya kuchakata mazao ya misitu
ambayo imenunuliwa na Program ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu
(FORVAC) kwa ajili ya wilaya ya Songea na Namtumbo. Wengine kutoka kulia
kwa Waziri ni Mwenyekiti wa CCM Addo Mwisho, Mkuu wa Wilaya ya
Namtumbo Sophia Kizigo, kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher
Ngubiagai, Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Isabela Chillumba na Mshauri Mkuu wa
Ufundi (CTA) FORVAC Juhan Harkonen.
Mkurugenzi
Mkuu wa Shirika la Mpingo na Maendeleo (MCDI), Makala Gaspar
akimuelezea Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk.Damas Ndumbaro namna
mashine ya kisasa ya kuchakata mazao ya misitu inavyofanya kazi.
NA SULEIMAN MSUYA, SONGEA
WAZIRI
wa Maliasili na Utalii Dk.Damas Ndumbaro amesema serikali inaendelea
kuhamasisha miradi ya kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu
kwa kuwa ina mchango mkubwa kwenye ukuaji wa pato la taifa.
Dk.Ndumbaro
amesema hayo wakati wa uzinduzi wa mashine ya kuchakata mazao ya misitu
iliyotolewa Shirika la Mpingo na Maendeleo (MCDI), chini ya ufadhili wa
Program ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC).
Program ya FORVAC inatekelezwa chini ya Idara ya Nyuki na Misitu na kufafhiliwa na Serikali ya Tanzania na Finland.
Amesema
kinachofanywa na FORVAC na MCDI ni sehemu utekelezaji wa Ilani ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM), Ibara ya 69 kigungu F ambayo inasema kuwepo
mashine za kuongeza thamani mazao ya misitu ili kuleta ajira na kusaidia
wananchi.
"Misitu ni
sekta muhimu sana katika nchi kimazingira, kiuchumi, ajira na ukuaji wa
viwanda. Leo tumezindua mashine hii inayochakata tani 5,000 kwa mwaka,
mbao 400 kwa siku ni kiwanda kabisa ambacho kinaongeza ajira, kodi na
pato la taifa kwa ujumla.," amesema.
Amesema
misitu nchini Tanzania inachukua asilimia 54 ya eneo lote hivyo
ikitumiwa kwa matumizi bora itabadilisha maisha ya wananchi.
Dk.Ndumbaro
amesema ili sekta hiyo kuendelea kuongoza katika uchangiaji wa pato la
taifa ni vema wadau wote kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha
taratibu zinafuatwa kwenye kila hatua muhimu kama FORVAC na MCDI
wanafanya.
Amesema kwa
sasa sekta hiyo inachangia pato la taifa kwa asilimia 21 ambapo Utalii
inachangia asilimia 17.5 na misitu asilimia 3.5 hivyo dhana ya mnyororo
wa mazao ya misitu itumike kuongeza mchango zaidi.
Waziri
Ndumbaro amesema miti na misitu ikivunwa kwa mfumo endelevu itachochea
maendeleo hivyo rai yake ni kuona kila wilaya yenye miti inayoweza
kuvunwa kiundelevu ikawa na mashine ya kisasa ya kuchakat mazao ya
misitu.
Amesema Serikali
itahakikisha kila mahali kwenye fursa za misitu inatumiwa kuchochea
maendeleo na huduma za kijamii na kuvitaka vijiji kununua mashine za
kuchakata.
Waziri amesema wao kama wizara hawatalala kuhakikisha mchango wao kwa pato la taifa unaongezeka.
"Niwaombe
wadau wote sekta ya misitu tafuteni Sera ya Misitu ya 1998 na Sheria ya
Misitu ya 2002 kuhakikisha lengo la sekta hii kuchangia pato la taifa
inatimia bila kuathiri mazingira na maliasili zingine" amesema.
Kwa
upande wake Mratibu wa FORVAC Kitaifa, Emmanuel Msoffe amesema
wamesukumwa kutoa fedha za ununuzi wa mashine hiyo ili usimamizi wa
misitu kuwa endelevu huku ukuaji wa uchumi ukiwepo.
Amesema
mashine hiyo ambayo imegharimu zaidi ya shilingi milioni 100 itatumika
katika vijiji vya Longosi, Lipagalo Liweta, Litoa, Litumbati vya wilaya
ya Songea na vijiji vitano vya wilaya ya namtumbo.
Amesema
program hiyo imekuwa na mafanikio kwa kiwango kikubwa katika hatua zote
ila kuna changamoto ya masoko na kuahidi kuziifanyia kazi.
Mkurugenzi
Mkuu wa MCDI, Makala Gasper amesema wamekuwa wakijishughulisha na
uhifadhi wa misitu kwa kushirikiana na Serikali katika kila ngazi jambo
ambalo linachangia mafanikio.
Amesema
mashine hizo zina mchango mkubwa kwenye kuongeza mnyororo wa thamani wa
mazao ya misitu ambapo hadi sasa vijiji 61 vimenufaika na kukusanya
zaidi ya shilingi bilioni 2 zinazotumika kwa miradi yaayaaendeleo.
"Tupo
katika vijiji 61 wilaya 9 na mikoa 4 ambapo kuna mabadiliko makubwa
katika kukuza kipato cha wanavijiji, kuboresha na kujenga huduma za
jamii, ajira kupatikana na manufaa mengine mengi," amesema.
Anasema
maratajio yao ni kuhakikisha jamii inayojihusisha na Usimamizi
Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ) inanufaika pamoja na Serikali.
No comments:
Post a Comment