Na Hamida Ramadhan
HIVI karibuni Katika kikao chake na waandishi wa habari Jijini Dodoma Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana, Patrobas Katambi amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), William Erio kuwasimamisha kazi watumishi wawili kwa kushindwa kuidai michango ya wafanyakazi wa kampuni ya Kiribo ya mkoani Mara, hadi kufikia deni la Sh.Bilioni 1.1.
Pia, ameagiza kusimamishwa kazi Ofisa Kazi wa Mkoa wa Tabora Revokatus Mabula kwa tuhuma ya matumizi mabaya ya madaraka.
Naibu Waziri huyo katika Ziara yake aliyoifanya Mikoa ya Kanda ya Ziwa amekiri na kusikitishwa na utendaji mbovu kwa watumishi wa Umma.
Aidha amewataja watumishi hao kuwa ni wa NSSF mkoani Mara ambao ni Maneno Mpogole na Abdulabi Salehe wanadaiwa kushindwa kutimiza majukumu yao kudai madeni kampuni hiyo hadi kufikia Sh.bilioni 1.1 huku ikionyesha fedha hizo zilikuwa hazifuatiliwi.
Amesema pia kuna kampuni ndogo zinazofanyakazi na mgodi wa North Mara zimekuwa na udanganyifu mkubwa na kuitolea mfano kampuni ya Kiribo kushindwa kulipa wafanyakazi zaidi ya Sh.milioni 300 na kukwepa kulipa kodi na fedha za mifuko ya hifadhi ya jamii hadi kufikia Sh.bilioni 1.1 na kodi ya sh. bilioni moja ambazo zingelipwa kwa Serikali.
"Naagiza mamlaka za Mkoa wa Mara kuufikisha Dodoma uongozi wa mgodi huo na mmiliki wa Kampuni hiyo ili kulipa madai hayo na kulipa kodi ya Serikali,"
Na kuongeza "Hawa watumishi wasimamishwe kazi ili uchunguzi ufanyike ni kwanini fedha hizo hazikufuatiliwa hadi kufikia Sh.bilioni 1.1 na kutoa onyo kwa mameneja wengine wa Mikoa kufuatilia madeni wanayodai kwenye taasisi za binafsi na za Serikali kuhakikisha madeni yanakusanywa kwa mujibu wa sheria,”amesema Katambi.
Kadhalika, amesema katika mgodi huo wa North Mara amebaini udanganyifu mkubwa hasa kwa wageni kufanyakazi bila kuwa na vibali vya kazi jambo ambalo ni kinyume cha taratibu za nchi.
“Pia nimekuta kazi wanazofanya zingeweza kufanywa na watanzania na taarifa inaonesha kazi hizo zinafanywa na wazawa, kulikuwa na udanganyifu mkubwa kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama tuliweka mtego na kubaini raia wa kigeni wakifanyakazi ambazo zingefanywa na wazawa,”amesema.
Amesema walinasa raia wa kigeni akifanya kazi za manunuzi na huduma za malipo na kubaini wengine tisa wakifanya kazi bila kuwa na vibali.
Ameagiza maombi yote ya vibali yaombwe kwa kamishna wa kazi ili kuepuka vishoka.
Kuhusu Ofisa Kazi wa Tabora, Katambi amefafanua kuwa Ofisa huyo wakati akiwa Mkoa wa Shinyanga kabla ya kuhamishiwa Tabora anatuhumiwa kushindwa kusimamia majukumu yake vyema.
“Nimebaini mtumishi huyo alikuwa akiwahujumu wafanyakazi na kuwa upande wa waajiri hivyo kushindwa kusimamia wafanyakazi na haki zao na kwamba baada ya kubaini mambo hayo nikiwa kwenye uchunguzi niligundua jioni ya siku hiyo aliita waandishi wa habari wasitoe habari hiyo,”amesema.
Hata hivyo, ameagiza Mamlaka iliyomteua kumchukulia hatua achukuliwe hatua kali iwe mfano kwa wengine.
Pamoja na hayo, Katambi katika ziara yake amebaini mgodi wa Elhilal wa Shinyanga kuna baadhi ya wafanyakazi 35 wa mgodi huo wanadai kampuni hiyo Sh.milioni 80 za michango iliyopaswa kuwasilishwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii(NSSF).
Kwa upande wake, Kaimu Kamishna wa kazi Andrew Hebron, ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na kiongozi huyo.
No comments:
Post a Comment