HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 19, 2021

Kikundi cha kuhifadhi na kutunza Mazingira cha CHAPAKAZI chamlilia Magufuli

 

NA HAMIDA RAMADHANI, DODOMA

 

WATANZANIA nchini wameendelea kuomboleza na kumlilia aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli aliyefariki Dunia Machi 17 Mwaka huu.

Licha ya Watanzania kupitia katika kipindi kigumu lakini wameonyesha wazi wazi kushtushwa na k ulizwa na kifo hicho ambapo kikundi cha Kuhifadhi na Kutunza Mazingira cha Chapakazi cha Jijini hapa kimesema kitaendelea kumlilia na kumkumbuka kwa wema aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk.John Magufuli kutokana na kutoa fursa kwa vijana wengi.

Pia, kimempongeza Rais Mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuapishwa jana kuwa Rais  ambapo kimedai kina imani ataendelea kuhakikisha analinda na kutunza mazingira nchini.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini hapa, Mtunza Fedha wa Kikundi hicho,Darwesh Said amesema wamepokea kwa masikitiko makubwa msiba wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema watamuenzi aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dk. Magufuli kwa kuchapa kazi kwani alitoa fursa kwa vijana wengi.

“Tunamlilia aliyekuwa  Rais wetu tumeumia sana kikubwa tunachoweza kusema tutaenzi yale mazuri yake kwa vitendo kwani alitaka watu kufanya kazi na sisi vijana tulifanya kazi kwa nguvu zote.Ametuwezesha kupata mikopo,ametuheshimisha sana vijana,”amesema.

Vilevile,amesema wataendelea kumkumbuka aliyekuwa Rais wa Tanzania Magufuli kwa kuhamishia Serikali Dodoma hali ambayo iliwapa nafasi ya kuuza miche mingi pamoja na kutengeneza bustani za watu mbalimbali.

“Baada ya kutangaza Serikali kuhamia Dodoma maisha yetu yalibadilika kila aliyekuja Dodoma alitaka eneo hivyo walipanda miti ya matunda na vivuli hali ambayo ilitusaidia kuongeza vipato,”amesema.

Amesema Magufuli amefanya vitu vingi na vya kukumbukwa ambavyo ni vizuri kwa Taifa na wananchi wanyonge katika kila sekta.

Katika hatua nyingine,Kikundi hicho kimempongeza Rais mpya Samia Suluhu Hassan kwa kuapishwa  kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema kikundi hicho kina imani nae katika  utendaji kazi wake hususani katika masuala ya utunzaji wa mazingira kutokana na kuwahi kuwa Waziri wa Muungano na Mazingira katika Serikali zilizopita.

“Sisi watu wa mazingira tupo pamoja na Mheshimiwa Rais Samia, na tutaendelea kuyatunza mazingira kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema.

No comments:

Post a Comment

Pages