Wakina mama wachuma uyoga asili,
Hilda Komba (katikati), Veronica Sakwaya (kulia) na Germana Clement wa
kwanza kushoto, kutoka kijiji cha Amani Makoro kata ya Amani Makoro
wilayani Mbinga mkoani Ruvuma wakichuma na kuandaa uyoga kwenye msitu wa
kijiji.
Mratibu wa FORVAC Kongani ya Ruvuma, Marcel Mutunda, akielezea namn program hiyo inachakata kupata vikundi vya kusaidiwa.
NA SULEIMAN MSUYA, MBINGA
VIKUNDI
na watu binafsi vipatavyo 20 kutoka katika vijiji saba vya wilayani
Mbinga mkoani Ruvuma wamepatiwa vifaa vya kuongeza mnyororo wa thamani
wa mazao ya misitu vyenye thamani ya shilingi milioni 100.
Hayo
yamesemwa na Mtaribu wa FORVAC, Kongani ya Ruvuma, yenye wilaya za
Nyasa, Mbinga, Namtumbo, Songea na Tunduru, Marcel Mutunda wakati
akizungumza na mwandishi wa habari hii.
Mutunda
amesema FORVAC inatekelezwa na Idara ya Misitu na Nyuki kupitia
ufadhili wa Serikali ya Tanzania na Finland ina lengo la kuhakikisha
mazao ya misitu yanakuwa kwenye mnyororo wa thamani na kuwanufaisha
wanavijiji.
Amesema
wamewezesha vikundi na watu binafsi vipatavyo 20 katika Wilaya ya Mbinga
kushiriki kwenye uhifadhi wa misitu kwa kuwekeza mizinga ya nyuki,
kuokota uyoga na wasusi wa makapu na nyungo hivyo vifaa vya kuchakata
mazao ya misitu vitaongeza thamani.
"Kwa
mwaka huu FORVAC imetoa shilingi milioni 100 kwa vikundi 20 ili
wanununua vifaa vya kuchakata uyoga, nyuki, nta, asali, makapu na nyungo
ambapo tumeingia mkataba na Sedet Vicoba ili wanunue vifaa hivyo.
Mfano
hapa katika kijiji cha Amani Makoro wanavikundi wameomba mitambo ya
kurina na kukamukia asali kama buti, nguo, chujio na vingine," amesema.
Mtatibu
huyo amesema pia wametoa pikipiki moja kwa Mzee Komba ambaye
anajihusisha na kuchukua mianzi ili atengeneze makapu na nyungo.
Amesema
wamewawezesha wakina mama watatu ambao wanajihusisha na uokotoji wa
uyoga ambao wamepatiwa mitambo ya kuchakata uyoga, nguo na buti ili
kujikinga na wadudu wabaya kama nyoka.
Amesema
vikundi vingine ambavyo vitapata vitendeakazi ni pamoja na Kijiji cha
Ukata, Kiwombi, Kindimba Juu, Kindimba Chini, Ndongosi na Barabara.
Akizungumzia ujio wa FORVAC wilayani Mbinga Ofisa Misitu wa wilaya hiyo Halifa Singano amesema program hiyo ina tija kwa jamii.
Singano
amesema kupitia program hiyo jamii imeinuka kiuchumi kwa kuwa wanatumia
misitu kuvuna mazao ambayo sio mbao kwa njia endelevu.
Amesema FORVAC imechochea uhifadhi, kuzuia uvunaji haramu na kuwafanya wananchi kutambua faida za misitu.
Ofisa
misitu huyo amesema katika kuhakikisha dhana ya FORVAC inasambaa
wameendelea kutoa elimu kwa wanavijiji kuunda vikundi ili wapate fedha
za halmashauri kusimamia misitu.
"FORVAC
imeleta mabadiliko makubwa ya kifikra kuhusu uhifadhi hivyo sisi
tutaendelea kutoa elimu ili vikundi na watu binafsi kushiriki katika
kulinda na kutunza misitu," amesema.
Ofisa
Mtendaji wa Kata ya Amani Makoro, Joachim Kaponda amesema program hiyo
imekuja wakati muafaka kwani misitu imeanza kulindwa.
"Ujio
wa FORVAC umeibua vikundi vinne vya Hapa Kazi Tu, Jitambue na vingine
hapa Amani Makoro ambavyo vinajihusisha na ufugaji wa nyuki na vingine
vinachuma uyoga hali ambayo inasadia wanakijiji kuwa na shughuli nyingi
za kufanya tofauti na zamani," amesema.
Amesema
wanaiomba FORVAC kuendelea kutoa elimu ili wanavijiji wengi kujiunga na
program hiyo muhimu ambayo itachangia ongezeko la kipato kwa wanavijiji
na Serikali.
Diwani wa
Kata ya Amani Makoro Ambros Nchimbi, amesema program hiyo imepunguza
utegemezi kwa wananchi wengi wa kata yake jambo ambalo linamrahisishia
ufanyaji kazi.
"Nina vijiji viwili vya Amani Makoro na Kiwombi ambao vinatumia msitu wa asili inayowazunguka kutekeleza shughuli zao," amesema
Wakizungumzia
ujio wa FORVAC wachuma uyoga asili Hilda Komba, Veronica Sakwaya na
Germana Clement wamesema program hiyo imeweza kubadilisha maisha yao
kiuchumi, kijamii na maendeleo.
Wamesema kupitia uchumaji wa uyoga asili wameweza kufanikisha mipango yao mingi bila kuwa wategemezi kwa waume zao.
"Sisi uyoga ni mkomboazi wa maisha yetu umetuondolea utegemezi tunawapongeza sana FORVAC kwa kutuwezesha," amesema.
Naye
Jackson Boimanda Mshauri wa Masuala ya Biashara kutoa Shirika la Sedet
amesema wao wamekuwa wakitoa elimu kwa vikundi ili kujua namna ya
kufikia malengo.
Amesema wanavijiji waliopo kwenye vikundi wameonesha uelewa katika kuomba fedha na vifaa jambo ambalo linawapa faraja.
No comments:
Post a Comment