Na Mwandishi Wetu, Mwanza
KATIBU Mkuu wa Chama cha Netiboli nchini (CHANETA), na mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa, Judith Ilunda, ambaye ni mchezaji wa timu ya Uchukuzi leo ameshindwa kuokoa jahazi lao lisizame baada ya kufungwa na Ikulu magoli 37-14 katika mchezo wa netiboli wa mashindano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika kwenye uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.
Ilunda aliyekuwa akicheza nafasi ya ufungaji akisaidia na Neema Mwanu waliipeleka timu yao mapumziko wakiwa nyuma kwa magoli 14-8. Wachezaji wengine wanaounda timu hiyo ni Neema Makassy, Habiba Othman, Mchilo Rajabu, Irene Mitava na Martha Kibona; wakati wachezaji wa Ikulu ni Restuta Boniface, Elizabeth Fussi, Irene Kivile, Chuki Kikalao, Sophia Komba, Salome Mika, Anna Msulwa, Amina Mwampole na Lilian Sylidion.
Katika mchezo mwingine timu ya Tanesco imewachapa bila huruma Wizara ya Mambo ya Nje kwa magoli 56-2. Washindi waliongoza kwa magoli 25-2 hadi mapumziko; Nayo timu ya Shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC) ilipata ushindi wa chee wa magoli 40 na pointi mbili baada ya wapinzani wao Ulinzi kutoonekana uwanjani.
Katika michezo ya soka timu ya Uchukuzi ilianza vyema kwa kuwafunga Wizara ya Mambo ya Nje kwa magoli 7-0 mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Nyamagana. Magoli ya washindi yalifungwa na Selemani Kaitaba na Idrisa Bahatisha kila mmoja kafunga (2); huku Salim Salehe, Lugano Mwasomola, Said Singano, na David Kunambi wamefunga bao moja kila mmoja.
Nayo timu ya Tanesco iliwaadhibu Ukaguzi kwa magoli 6-0. Magoli ya Washindi yalifungwa na Kurwa Mangarano magoli matatu, huku Ndere Maketa, Khalifa Shekule na Castory Mhemchele wote wamefunga bao moja.
Timu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) iliwafunga wenyeji timu ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza (RAS Mwanza) kwa magoli 4-2. Wafungaji wa NCAA ni, hukuTumaini Sendemu magoli mawili, Liberatus Rwechungu na Regan Peter wamefunga goli moja kila mmoja.
Kwa upande wa michezo ya kuvuta Kamba iliyochezeshwa na waamuzi Dotto Andrea na Rajabu Shekimweri, timu ya wanaume ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro iliwavuta Ukaguzi mivuto 2-0; pia kwa upande wa dada zao waliwavuta Wizara ya Kilimo kwa mivuto 2-0; wakati katika mchezo wa wanawake Taasisi ya Saratani Ocean Road ilipata ushindi wa chee wa mivuto 2-0 baada ya Wizara ya Mambo ya Nje kuingia mitini.
Michuano hiyo inaendelea kesho ambapo katika soka zitakazofanyika kwenye uwanja wa CCM KIrumba timu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) watakutana na Ulinzi; huku Wizara ua Mambo ya Nje watacheza na Wizara ya Mambo ya Kilimo; wakati katika uwanja wa Nyamagana timu ya Ukaguzi watakutana na Mamlaka ya Majisafi na taka Mwanza (MWAUWASA).
Katika michezo ya netiboli ambayo yote inafanyika CCM Kirumba timu ya Mamlaka ya Majisafi na taka Mwanza (MWAUWASA) watapepetana na Tanesco; nao Ulinzi watawakaribisha Wizara ya Kilimo; nayo Wizara ya Mambo ya Nje watacheza na ndugu zao Wizara ya Mambo ya Ndani.
Nayo michezo ya kuvuta Kamba wanawake timu ya Uchukuzi itakutana na Tanesco, huku Mamlaka ya Majisafi na taka Mwanza (MWAUWASA) itacheza na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC); wakati kwa upande wa wanaume Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) watavutana na Tanesco na mchezo mwingine Wizara ya Mambo ya Nje watakutana na Wizara ya Kilimo.
Fainali za michezo ya soka, netiboli na kuvuta Kamba zinatarajia kufanyika tarehe 29 Aprili, 2021 kwenye uwanja wa CCM Kirumba.
No comments:
Post a Comment