HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 10, 2021

WAZIRI CHAMURIHO ATAKA TAASISI ZA UJENZI, UCHUKUZI KUWAJIBIKA


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mheshimiwa Dkt. Leonard Chamuriho, akizungumza na Wakurugenzi wa Wizara, Wakuu wa Vitengo,  pamoja na Viongozi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara yake (hawapo pichani), katika kikao kazi kilichofanyika jijini Dodoma. Kulia ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mheshimiwa Mwita Waitara.


Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mheshimiwa Mwita Waitara, akisisitiza jambo katika kikao kazi kilichowakutanisha Wakurugenzi wa Wizara, Wakuu wa Vitengo pamoja na Viongozi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo jijini Dodoma. Kushoto ni Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mheshimiwa Dkt. Leonard Chamuriho. 

 

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, amewataka Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara yake kuhakikisha wanaandaa taarifa kila mwezi zinazoelezea utekelezaji wa majukumu yao ili kusaidia Wizara kufahamu kwa undani utendaji wa Taasisi hizo ikiwemo mafanikio na changamoto zake.

Hayo aliyasema Waziri huyo, jijini Dodoma, katika kikao kazi cha kumtambulisha Naibu Waziri wa Wizara hiyo  Mhe. Mwita Waitara, kwa mara ya kwanza kwa viongozi wa Taasisi hizo ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza kuwa Wizara itakuwa inaandaa vikao kama hivyo  mara nne kwa mwaka ili kujadiliana kwa pamoja na kupata tathmini na  mwelekeo wa Wizara katika ufanisi wake wa utendaji kazi.


"Nimeamua leo kuitisha kikao hiki ili kumtambulisha Naibu Waziri kwa wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara yangu, pia kukumbushana kuhusu utekelezaji wa masuala mbalimbali yaliyo katika Taasisi zao", amesema Waziri Chamuriho.

Aidha, Chamuriho amezisisitiza Taasisi hizo kushirikiana na kuwajibika ipasavyo katika miradi wanayoitekeleza kwani mingi huigusa jamii ambapo ameongeza kuwa, kufanya hivyo kutapelekea maendeleo kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe.Mwita Waitara, amewataka viongozi hao wa Taasisi kumpa ushirikiano wa kutosha na kwamba ofisi yake itakuwa wazi kwa ajili ya kupokea ushauri na maoni mbalimbali  lengo likiwa ni kusaidia kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyo chini ya Wizara hiyo ili kuleta maendeleo kwa wananchi.

“Naomba Wakuu wa Taasisi wanipe tu ushirikiano wa kutosha na niwabainishie kuwa Ofisi yangu itakuwa wazi wakati wote kwa ajili ya kupokea ushauri lengo likiwa ni kuleta tija na maendeleo kwa wananchi”, amefafanua Naibu Waziri Waitara.

Naye, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi, Arch.Edwin Nunduma,  amesema kuwa agizo hilo la Waziri la kuleta taarifa za utekelezaji Wizarani litawafanya kuwajibika zaidi kutokana na kuwa Wizara itafuatilia kwa karibu utendaji wao.

"Utaratibu huu ni mzuri, kwani hata changamoto zikitokea itakuwa ni rahisi kuzitafutia ufumbuzi mapema na kwa haraka kuliko kusubiri kuleta taarifa ya robo mwaka  kwa kila kota kama ilivyo awali", amesema Nunduma.

Kikao hiki cha siku moja ambacho kimemkutanisha Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mheshimiwa Dkt. Leonard Chamuriho, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe.Mwita Waitara, Menejimenti ya Wizara hiyo pamoja na viongozi wakuu wa Taasisi 23 zilizo chini ya Wizara hiyo , kilikuwa na lengo la kutambuana na kukumbushana kuhusu uwajibikaji katika Taasisi zao.

No comments:

Post a Comment

Pages