Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt. Saada Mkuya Salum, amesema ofisi yake itasimamia vyema majukumu yake ili kuhakikisha masuala yote mtambuka yanakuwa salama na hayaathiriwi.
Ameeleza
hayo wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa programu za ofisi yake
kwa kipindi cha miezi mitatu Januari na Machi 2021 aliyoiwasilisha kwa
Kamati ya inayosimamia Ofisi za viongozi wakuu wa Kitaifa ya Baraza la
Wawakilishi Dkt Saada amesema Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais moja
kati ya malengo yake ni kuhakikisha inakuwa na mfumo bora wa kisera na
kisheria kwa taasisi inazozisimamia.
Aidha amesema kupitwa na muda kwa baadhi ya Sera na Sheria zinazosimamiwa na Ofisi ya
Makamu wa Kwanza wa Rais ni changamoto ambayo tayari imeanza kufanyiwa
kazi, kufanyiwa mapitio na kutoa mapendekezo ya kurekebisha Sera na
Sheria hizo kwa ajili ya utekelezaji ili kuendana na kasi ya kiutendaji
kwa mujibu wa taratibu.
‘Rasimu ya Sera ya Dawa za
Kulevya imeandaliwa na ipo katika hatua ya kuwasilishwa Baraza la
Mapinduzi. Rasimu ya Sera ya Mazingira ipo katika hatua ya maandalizi na
rasimu ya marekebisho ya Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ipo katika hatua
ya kupelekwa kwa wadau’alifafanua Dkt. Saada.
Nae
Mwenyekiti wa Kamati ya inayosimamia Ofisi za viongozi wakuu wa Kitaifa
ya Baraza la Wawakilishi Mhe Hassan Khamis Hafidh ameiomba Ofisi ya
Makamu wa Kwanza wa Rais kuhakikisha wanasimamia vyema majukumu yao ili
Zanzibar iendelee kuwa salama kwa masuala wanayoyaratibu.
Hassan
amesema Zanzibar inahitaji kuwa salama katika kulinda na kuhifadhi
mazingira, kutokubali kuwa ni sehemu ya wapitishaji na wauzaji na
wasambazaji dawa za kulevya, kuzingatia vyema masuala ya upatikanaji wa
haki za Watu wenye Ulemavu na kuwa na jamii isiyokuwa na maambukizi ya
virusi vya Ukimwi na UKIMWI.
Aidha amewataka viongozi wa Ofisi hio kuhakikisha matumizi na mapato yanaendana na utekelezaji wa mpango wa bajeti.
Akitoa
maelezo ya mradi wa kujenga uwezo wa kuhimili na kukabiliana na athari
za mabadiliko ya tabia nchi kwa maeneo ya pwani katika eneo la
Kilimani Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Bi Khadija Khamis
Rajab amesema mafaniko makubwa yamepatikana katika mradi huo ambapo
hifadhi ya fukwe imerudi ukilinganisha awali maji yalikuwa yakiingia
karibu na maeneo ya makaazi.
Mradi huo ambao
umefadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa kimazingira ulianza 2013 - 2018 na
shughuli zilizofanyika katika kurudisha mazingira ni upandaji wa mikoko
na kuweka ukuta kwa kutumia mawe kwa ajili ya kuzuia maji ya bahari
yasipande juu na kuathiri maeneo ya makaazi ambapo shughuli hizo
zimegharimu zaidi ya dola za kimarekani laki 4 zilizosimamiwa na
wahisani wenyewe.
Aidha katika kuliendeleza eneo
mradi ulipewa Jumuiya ya kuhifadhi na kusimamia mazingira ZACEDY na
hatua kadhaa zilichukuliwa ikiwemo kutoa elimu kwa jamii, viongozi wa
Wilaya na Shehia ili wapate uelewa, usafishaji wa eneo, masuala ya
ufatiliaji na tathmini, shughuli za upandaji miti ambapo gharama
zilizotumika ni zaidi ya Milioni 11.
Katibu wa
Jumuiya inayosimamia mazingira ZACEDY kupitia eneo la mradi wa kujenga
uwezo wa kuhimili na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi
kwa maeneo ya pwani katika eneo la Kilimani ndugu Jamal Khamis Juma
amesema kwa kiasi kikubwa wamefanikiwa kurudisha eneo hilo kwa
kushirikiana na Ofisi ya Wilaya Mjini na wanajamii
Pia
ametoa shukurani kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Idara ya
Mazingira na Mamlaka ya usimamizi wa Mazingira kwa kuaminiwa na
kuliendeleza eneo hilo.
Ndugu Jamal amesema
chagamoto kubwa katika eneo hilo kwa sasa ni kutumika kwa shughuli
mbalimbali za kijamii, baadhi ya watu wasiowaaminifu kuiba miti
wanayootesha ikiwemo mikoko na mivinje na kuiomba Kamati kuweza kusaidia
kupata wafadhili ili waweze kuendeleza mradi huo ambao kwa sasa
umemeliza muda wake.
Kamati
ya inayosimamia Ofisi za viongozi wakuu wa Kitaifa ya Baraza la
Wawakilishi Zanzibar awali ilitembelea na kukaguwa mradi wa kujenga
uwezo wa kuhimili na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi
kwa maeneo ya pwani katika eneo la Kilimani kisha kuonana na kufanya
mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe. Othman Masoud Othman pamoja
na kupokea na kuipitia taarifa ya utekelezaji wa programu za ofisi
yake kwa kipindi cha miezi mitatu Januari na Machi 2021.
No comments:
Post a Comment