AFISA Lishe Mtafiti kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Fatma Mwasora amesema kuwa Kama mtu atakula futari, daku ahakikishe chakula hicho kinakuwa ni mlo kamili ambao unatokana na makundi matano ya vyakula.
Futari ni kile chakula au mlo ambao mara nyingi hutayarishwa katika kipindi cha kufunga mwezi Mtukufu wa Ramadhani na daku ni mlo ambao hupaswa kuliwa wakati wa usiku kabla ya funga inayofuatia.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Mwasora amesema kuwa wanasisitiza ulaji huo kwani kumekuwa na tabia katika kipindi cha mfungo wa Ramadhani watu wengi huwa wanaangalia vyakula kutoka kundi moja ambalo linahusisha vyakula aina ya nafaka na mizizi.
Afisa huyo Mtafiti amefafanua kuwa kwenye kundi la mizizi ni viazi vitamu, mviringo mihogo na ndizi mbichi kisayansi hilo ni kundi moja.
" Hata vile virutunishi ambavyo tunavipata vinatokana na kundi moja hivyo kusababisha hukosekana vingine vinavyotokana na makundi mengine ya vyakula," ameongeza.
Imekuwa ni mazoea kwa Waislamu katika mfungo akili yetu futari ni lazima iwe ni chakula kinachotokana na mizizi au nafaka," amesema Mwasora.
Ameongeza kuwa vyakula hivyo mara nyingi vinapoliwa mwili hupata nishati lishe au wanga kwa ajili ya kuupatia mwili nguvu na joto tu na kukosa virutubishi toka kwenye makundi mengine.
" Vyakula hivi sisi tunaona ndio vyakula vya futari ukiangalia uji unatokana na nafaka, kwenye futari utakuta tambi wakati nayo imetoka katika kundi hilo hilo tunapata virutunishi vya aina moja vya nishati lishe, " amesema Mtafiti huyo.
Amesema kuna athari zake iwapo mtu atakula kundi moja la chakula ambavyo ni vyakula vya vinavyotokana na nafaka na mizizi tu, kwani atakosa vyakula vya aina ya Protini, vitamini na madini ambavyo ni muhimu katika kujenga mwili na kuimarisha kinga mwili.
Aidha amewataka Waislamu kula vyakula vinavyotokana na makundi yote matano ili kukamilisha mlo kamili, ambao ni vyakula vya aina ya nafaka, mizizi na ndizi mbichi, jamii ya mikunde na nyama na vile vinavyotokana na mboga mboga na matunda na kwa kiasi vile vinavyotokana na sukari na mafuta.
No comments:
Post a Comment