HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 30, 2026

Benki ya CRDB yatoa Elimu ya Fedha kwa Wabunifu wa Mitindo

BENKI ya CRDB imewakutanisha zaidi ya Washonaji na Wabunifu wa Mitindo nchini kwa lengo la kuwapatia elimu ya fedha kuwawezesha kukuza biashara zao, kutoa ajira kwa vijana na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Meneja wa Huduma kwa Wateja wa Benki ya CRDB, Jafari Hassanali, amesema tasnia ya mitindo ipo katika safari ya kutoka kwenye kipaji cha kawaida na kuelekea kuwa biashara endelevu yenye mchango mkubwa katika uchumi wa taifa.

Amesema ubunifu ulio sambamba na maarifa ya biashara na usimamizi wa fedha ni msingi muhimu wa kushikilia na kuimarisha uchumi wa nchi, akibainisha kuwa sekta ya ubunifu ni miongoni mwa sekta zinazokua kwa kasi na zenye uwezo mkubwa wa kutoa ajira kwa vijana.

Akizungumza katika Jukwaa la Tanzania Fashion Forum, Hassanali amewataka wabunifu kutumia mikopo kama nyenzo ya uwezeshaji wa biashara badala ya kuifanya kuwa mazoea.

“Unapokopa lazima uelewe kuwa mkopo ni uwezeshaji, si mazoea. Wabunifu mnapotaka kukopa hakikisheni mna oda au kazi zinazoihitaji fedha hiyo ili kukamilisha,” amesema.

Ameongeza kuwa wakopaji wanapaswa kujiuliza lengo la mkopo kabla ya kukopa, akisisitiza kuwa mikopo isiyotumika kukuza biashara huua maendeleo ya mjasiriamali.

“Mkopo haupaswi kutumika kwa matumizi binafsi. Ukikopa pesa ya kulipa madeni mengine au matumizi yasiyoendeleza biashara, huo si uendelezaji bali ni kuua biashara,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Fashion Association of Tanzania (FAT), Mustapha Hassanali, amesema Jukwaa la Mitindo Tanzania ni jukwaa muhimu linaloangalia mitindo si kama suala la urembo pekee, bali kama nguzo ya uchumi, ajira, biashara, utambulisho wa taifa na nafasi ya Tanzania katika soko la dunia.

“Ni heshima na dhamana kubwa kusimama mbele yenu leo. Mitindo leo si maonesho ya mavazi tu, bali ni sekta ya kiuchumi inayohitaji miundombinu, mifumo ya kibiashara na uzalishaji,” amesema.

Ameeleza kuwa kwa muda mrefu mitindo barani Afrika imeonekana kama sanaa pekee, huku ikikosa mifumo madhubuti ya kibiashara, viwanda na uzalishaji, hali iliyokwamisha mchango wake katika uchumi.

Akiwakilisha sekta ya ubunifu kupitia Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), amesema majadiliano hayo yanalenga kuwakutanisha wabunifu, taasisi za fedha, sekta ya elimu, viwanda na watunga sera ili kupata suluhisho za vitendo zitakazowezesha tasnia hiyo kukua kiviwanda.



Amebainisha kuwa nchi kama Italia, Uturuki na Morocco hazikufanikiwa kwa bahati mbaya, bali kwa kuwekeza kwenye mifumo na kuirasimisha tasnia ya mitindo, hatua iliyoiwezesha kuwa chanzo kikubwa cha mapato na ajira.
“Tanzania ina vipaji vingi kuanzia wabunifu wa mitaani hadi wa kimataifa.

 Tunachohitaji ni mjadala wa vitendo, si nadharia, ili kubadilisha kipaji kuwa sekta imara ya viwanda,” amesema.




No comments:

Post a Comment

Pages