HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 07, 2021

NMB yaboresha bima ya faraja, yatambulisha bima ya vikundi


Mkuu wa Kitengo cha Bima cha Benki ya NMB, Martine Massawe akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam kuhusiana na Bima ya Maisha. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Metropolitan Life (CEO), Amani Boma na kulia ni Meneja Mkuu wa Biashara ya Makampuni Sanlam, Nura Masood. (Na Mpiga Picha Wetu).

 

Na Mwandishi Wetu

 

KWA mara nyingine Benki ya NMB imedhihirisha kauli mbiu yake kuwa ipo karibu na wateja, imekuja na maboresho ya huduma zake za bima ili kuhakikisha Watanzania wanapata faraja wakati wa matatizo.

Benki hiyo inashirikana na kampuni mbili za bima, Metropolitan Life na Sanlam Life ambapo watakuwa na utaratibu wa kutoa bima za maisha na vikundi kwa wateja na wasio wa NMB, katika kuangalia matarajio ya wateja wao baadae ikitokea hatari katika maisha yao na hivyo kusaidia malengo ya wateja kufikiwa hata kama wao hawapo au wamepata ulemavu.

Akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya NMB jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Idara ya Bima NMB, Martine Massawe alisema wameiboresha huduma ya bima ya NMB Faraja kwa kuongezea kiasi cha fedha kinachotolewa lakini pia kuongeza kpengele cha ulemavu wa kudumu atakaopata mteja pia atalipwa lakini pia wamekuja na hudma mpya ya bima kwa vikundi.

“”Katika kuchangia maendeleo ya bima nchini na kuisaidia serikali katika mikakati ya kuongeza idadi ya watumiaji wa huduma za bima, tumekuja na maboresho ya NMB Faraja lakini pia tuna aina mpya ya bima zitakazopatikana kwenye matawi yetu yote nchini,” alisema Massawe na kuongeza:

“Kuanzia Mei Mosi, 2021 NMB kwa kushirikiana na Sanlam tumefanya mabadiliko kwa kuongeza faida zaidi kwa wateja wetu. Mkono wa pole sasa ni mpaka Shilingi Milioni 2 kwa mteja, Sh Mil 2 kwa mwenza na pia Sh Mil 2 kwa mteja wetu atakapopata ulemavu wa kudumu. Hii ina maana kuwa unapomiliki akaunti ya NMB unapata faida ya kuwa na bima hii ya maisha na ulemavu wa kudumu (Faraja) bia gharama yoyote.”

Aidha, akizungumzia bima ya vikundi, Massawe alisema bima hiyo ni mpya sokoni ambayo itasaidia vikudi vyote ambavyo ni rasmi na visivyo rasmi: “Kikundi chochote kinaweza kuja na kukata bima na ikiwa mwanakikundi amefariki bima italipa gharama zote za mazishi ya mwanakikundi na familia yake, ikiwemo mwenza na watoto wasiozidi wanne. Mfano kikundi cha shule, Vikoba, Vikundi vya Whatsapp, Vikundi vya ukoo, vya familia na vikundi vingine vingi.”

Alibainisha, kikundi kinatakiwa kuwa na wanachama wasiopungua 10, mchango kwa mwezi upo wa aina tatu kuanzia Shilingi 500, Sh 1200 na Sh 2000 kwa kila mwanachama.

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya bima ya Metropolitan Life, Amani Boma alisema wamefikiria aina hiyo ya bima ya vikundi ili kuingia kwenye viatu vya watu wengi. Kwa kuwa vipo vikundi vinachangishana fedha nyingi kwa mwaka lakini kupitia utaratibu walioshirikiana na Benki ya NMB wanachama watalipa fedha kiasi kwa huduma kubwa.

“Tumeamua kuangalia nyanja zote za maisha katika vikundi, kama tunavyofahamu kinaweza kumkuta mtu yeyote wakati wowote, unaweza kuwa hujajiandaa lakini bima hii itakusaidia. Tena tumeamua iwe inalipwa ndani ya saa 48, kwa kuwa tunafahamu wapo wanavikundi wa imani mbalimbali za dini ambao utaratibu wao wa kuzikana unatofautiana,” alisema Boma.

Naye Meneja Mkuu wa Kampuni ya bima ya Sanlam (General Manager - Corporate Business), Nura Masoud alisema wamekuwa na ushirikiano na benki ya NMB katika bima kwa miaka zaidi ya 10, hivyo anaamini maboresho haya yatawavutia zaidi wateja wao.

Katika hatua nyingine benki ya NMB imeangalia kwa jicho pana sekta ya bima nchini kuwa na mchango mdogo kwenye pat la taifa, hivyo kwa ubunifu huu itasaidia kukuza sekta ya bima na kuruhusu watu wengi zaidi wa vipato mbalimbali kuwa na bima.

No comments:

Post a Comment

Pages