HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 03, 2021

Waandishi wa Habari waaswa

NA HAMIDA RAMADHANI, DODOMA

KATIKA kuadhimisha siku ya uhuru wa Vyombo vya habari waandishi wa habari nchini wametakiwa kujiendeleza na  masomo, ili kuweza kukuza ufanisi wa utendaji kazi jambo ambalo litasaidia kuondoa uholela wa watu ambao hawana taaluma. 

Aidha taaluma yoyote ni lazima iwe na misingi ambayo itamuongoza mwana taaluma katika utekelezaji wa majukumu yake awepo kazini.

Akizungumza leo jijini hapa Katibu mkuu wa chama cha waandishi  wa habari mkoani Dodoma Central Press Club (CPC) Ben Bago amesema waandishi wasipojiendeleza hawawezi kuwa na Taaluma.

"Imekuwa ni mtindo kawaida kwa kila mtu ambaye anaweza kupiga picha za harusi basi naye anakuwa mwandishi jambo ambalo ni kinyume na misingi na sheria ya taaluma ya habari lakini kupitia sheria hii ya habari ya mwaka 2016 ya waandishi kurudi kusoma sheria italindwa ," .

Na kuongeza kuwa "Nikweli maslahi ni duni lakini suala zima la kujiendeleza ni muhimu ili kupunguza utitiri wa watu wasiokuwa wanataaluma kwenye tasinia ya habari," amesema Bago

Aidha akizungumzia siku ya uhuru wa vyombo vya habari amesema siku ya uhuru wa vyombo vya habari ni kioo na inapofika siku hiyo waandishi wote wanapaswa kujiangalia wapi walipotoka na wanapokwenda sasa.

Amesema lengo kubwa la kuwepo kwa siku hiyo ni kumsaidia mwandishi wa habari kuweza kutafuta habari ,kufanya habari bila kunyimwa uhuru wake.

Sambamba na hayo akizungumzia suala la baadhi ya viongozi kutotoa ushirikiano kwa waandishi mpaka wengine kufikia maamuzi ya kuwaweka ndani waandishi wa habari amesema huo ni ulevi wa madaraka.

"Mfano mzuri ni kile kitendo alichokifanya yule mkurugenzi wa halmshauri  ya Temeke ule ni ulevi kama mtu anashindwa kutoa taarifa atafute mtu ambae atakua ndio mtoa taarifa ndio maana ya uwepo wa maafisa habari "amesema Bago

Naye Ronald Sonyo mwandishi wa habari jijini hapa amesema inapoadhimishwa siku hii ya uhuru wa vyombo vya habari waajiri pia watumie  siku hii kutambua mchango wa wana habari kwa kutoa mikataba na ajira.

"Tunasema hakuna vyombo vya habari bila mwandishi wa habari,hakuna mwandishi wa habari bila vyombo vya habari na hakuna habari bila mwandishi wa habari,kwahiyo waajiri wetu tunategemeana mtujali kwenye maslahi ili mtutengenezee mazingira rafiki ya ufanyaji kazi"amesema Sonyo


Hata hivyo Chama cha Waandishi wa Habari kwa Mkoa wa Dodoma kimepanga kufanya maadhimisho hayo Mei 8 ambapo watakutana na wadau mbalimbali kuzungumzia mipango, changamoto  yanayowahusu waandishi wa habari.





No comments:

Post a Comment

Pages