HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 25, 2021

WAZIRI AWESO ATOA ONYO KALI JUMUIYA ZA MAJI, AJA NA SULUHISHO LA KUMALIZA CHANGAMOTO


WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso,ameagiza kuvunjwa kwa Jumuiya ya Maji katika kijiji cha Berege wilayani Mpwapwa huku akitoa onyo kali la ubadhilifu wa fedha za Jumuiya ya watumia maji katika mradi wa maji kijijini hapo.

Kauli hiyo ametoa Mhe.Aweso wakati wa  ziara yake ya kukagua utekelezaji na uendeshaji wa miradi ya maji pamoja na kuzungumza na wananchi katika kijiji cha Berege kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa.

Waziri Aweso alipokea malalamiko ya wananchi kuhusiana na jumuiya ya watumiaji maji katika Kijiji cha Berege  kuwa fedha zinakusanywa bila ya kupelekwa benki na hivyo kulazimika kuivunja jumuiya hiyo.

Waziri Aweso amesema kuwa Jumuiya za Watumia Maji nchini zimekuwa na changamoto kubwa kwenye usimamizi wa miradi na matumizi sahihi ya makusanyo ya fedha;
amesisitiza na kutoa wito nchi nzima ikiwa ni suluhisho la kudumu la changamoto hii kuwa kuanzia sasa Jumuiya zote za watumia maji nchini ziwe na mafundi sanifu wanaotokana na Chuo cha Maji na kuwa na Watu wenye sifa ya Uhasibu na tayari Wizara imeingia makubaliano na Chuo hiki.

Pia  amemuagiza Meneja wa RUWASA Mpwapwa, Mhandisi Syprian Warioba kurejesha fedha zilizochukuliwa katika Jumuiya ya Watumia Maji Berege kuwalipa wataalam kwa ajili ya usimamizi wa miradi kwa kuwa serikali imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kazi hiyo.

Hata hivyo amemuagiza Meneja wa Wakala wa Uchimbaji Visima (DDCA) Peter Mdalangwila kuhakikisha wanafika Mpwapwa Jumamosi Mei 29, 2021 kuchimba visima vitatu katika Wilaya hiyo na kati ya visima hivyo kimoja kichimbwe katika Shule ya Sekondari Berege ili kupunguza adha ya maji inayowakabili wanafunzi shuleni hapo.

No comments:

Post a Comment

Pages