HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 01, 2021

Miezi mitatu ya baridi, upepo Tanzania

Na Irene Mark

MIKOA ya Mbeya, Iringa, Songwe, Njombe na Kusini mwa Morogoro inatarajiwa kuwa na baridi kali hadi kufikia chini ya nyuzi joto sita mwezi Julai.

Hata hivyo maeneo kati ya nchi mikoa ya Dodoma na Singida  yanatarajiwa kuwa na kiwango cha chini cha joto la kawaida ambacho ni kati ya nyuzi joto 11 hadi 14 kikiambatana na vipindi vya upepo mkali.

Akizungumzia mwelekeo wa Hali ya Hewa kwa kipindi cha Juni, Julai na Agosti (JJA) hapa nchini, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi amesema mifumo inaonesha kuwepo kwa joto la kawaida kwa ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi na chini ya kawaida kwa maeneo ya Nyanda za juu kusini magharibi na maeneo ya miinuko.

“Vipindi vya baridi kali vinatarajiwa kujitokeza katika mwezi wa Julai... hasa maeneo ya miinuko ya nyanda za juu kusini magharibi na vitakuwepo zaidi nyakati za usiku na asubuhi,” anasema Dk. Kijazi.

Amesema kandq ya Ziwa Victoria mikoa ya Mwanza. Geita, Kagera, Simiyu na Shinyanga, kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa cha kawaida hadi juu ya kawaida kati ya nyuzi joto 14 hadi 19.

Kuhusu Pwani ya Bahari ya Hidi, Dk. Kijazi ambaye pia ni Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani, amesema mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, visiwa vya Unguja na Pemba na maeneo la Kaskazini mwa mkoa wa Morogoro inatarajiwa kuwa na joto la hadi juu ya kawaida kwa nyuzi joto kati ya 18 na 23.

“Ukanda wa nyanda za juu kaskazini mashariki mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara kwa ujumla kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa hadi juu ya kawaida kwa nyuzi joto kati ya 10 na 17 kwenye maeneo mengi.

“...Kanda ya Magharibi mikoa ya Rukwa, Tabora, Kigoma na Katavi inatarajiwa kuea na joto la chini ua kawaida hadi juu ya kawaida kwa nyuzi joyo 13 na 19 kwa maeneo mengi,” amesisitiza Dk. Kijazi.

Kwa mujibu wa TMA, ukanda wa Pwani ya Kusini mikoa ya Lindi na Mtwara inatarajiwa kuwa na hali ya joto kati ya nyuzi joto 18 na 23 katika maeneo mengi ya mikoa hiyo.

Dk. Kijazi amesema, hali ya ukavu, upepo na ubaridi inaweza kusababisha athari kwa binadamu, wanyama na mazao hivyo kuzishauri mamlaka na wadau wa sekta mbalimbali kuchukua hatua za tahadhari ikiwemo kuzingatia matumizi mazuri ya maji na kujikinga ili kupunguza athari mbaya zinazoweza kujitokeza.

No comments:

Post a Comment

Pages