Zitto Kabwe akiwa na mshindi wa Uchaguzi wa Zambia Hakainde Hichelema, picha ilipigwa mwaka 2016.
Chama cha ACT Wazalendo kimemtumia Salaam za pongezi Rais Mteule wa Zambia, Ndg. Hakainde Hichilema kwa kuchaguliwa kuwa Rais mpya wa Jamhuri ya Zambia.
Taarifa ya Idara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya chama hicho leo Agosti 15,2021 imesema kwa kuzingatia matokeo rasmi yaliyokwishatangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zambia (ECZ) na baada ya Rais Edgar Lungu kukiri kushindwa ni dhahiri kuwa Ndugu Hakainde Hichilema ambaye ni mgombea wa chama cha upinzani cha UPND amevuka wigo wa zaidi ya asilimia 50 (50%+1) ya kura zote.
Taarifa hiyo ya ACT Wazalendo iliyosainiwa na Mkuu wa Idara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Fatma Abdulhabib Ferej imesema kwa matokeo hayo, Hakainde Hichilema ameshinda uchaguzi huo mkuu na kumuacha mbali mgombea aliyekuwa akitetea nafasi hiyo ya Urais, Ndugu Edgar Chagwa Lungu.
"Sisi ACT Wazalendo tukiwa ni Chama kiongozi wa Upinzani nchini Tanzania na Chama rafiki wa Chama cha UPND, tunampongeza Ndugu Hakainde Hichilema kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa saba wa Jamhuri ya Zambia.
"Ni matumaini yetu kuwa, chini ya uongozi wa Hakainde Hichilema, nchi zetu mbili- Tanzania na Zambia, zitashamirisha na kuimarisha uhusiano wa kihistoria katika nyanja za kiuchumi, miundombinu na kikanda kupitia Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC)." Ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha ACT Wazalendo kimemtakia mafanikio Rais huyo mpya katika majukumu yake mapya ya kuitumikia Zambia na hivyo kutimiza matakwa ya wananchi wa nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment