HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 16, 2021

NMB Marathon 2021 yazinduliwa, mapato kutibu wagonjwa Fistula CCBRT

 

 

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna na Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi (wa pili kushoto) wakitiliana saini mkataba wa ushirikiano wa mbio za NMB Marathon zenye lengo la kuchangia bilioni mmoja ndani ya miaka minne kwa ajili ya kuwatibu akinamama wenye Fistula. Kulia ni  Afisa Mtendaji Mkuu wa Bima UAP, Nelson  Rwihula na kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Sanlam Life Insurance,  Julius Magabe.




 

 


NA MWANDISHI WETU

BENKI ya NMB, imesaini makubaliano ya ushirikiano na Hospitali ya CCBRT, yanayolenga kukusanya kiasi cha Sh. Bilioni 1 (katika kipindi cha miaka minne) za matibabu ya Fistula kwa kina mama wasio na uwezo, kupitia Mbio za Hisani za NMB Marathon, zitakazofanyika kwa mara ya kwanza Septemba 18, 2021 jijini Dar es Salaam.

Kupitia NMB Marathon, ambazo mwaka huu zitafanyika chini ya kaulimbiu ya: 'Mwendo wa Upendo,' Benki ya NMB na CCBRT wanatarajia kukusanya zaidi ya Sh. Milioni 250 (kila mwaka), ambazo zitasaidia matibabu ya wagonjwa 60 wa Fistula, miongoni mwa mamia ya kina mama wanaoteseka kwa maradhi hayo.

Akizungumza wakati wa utilianaji saini wa makubaliano na uzinduzi wa mbio hizo, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, alisema kuna kila dalili za kufikia lengo la makusanyo hayo, hasa kutokana na uungwaji mkono waliopata kutoka Kampuni za Bima za Sanlam na UAP, ambazo zimechangia Sh. Milioni 100 (sawa na Sh. Mil. 50 kila moja).

Zaipuna alibainisha kuwa, Fistula Ni maradhi yanayotesa kina mama wengi nchini, na akawataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kujisajili kushiriki mnio hizo, ili kufanikisha lengo la makusanyo na matibabu ya wagonjwa wasio na uwezo wa kumudu gharama.

"Lengo ni kukusanya Sh. Bilioni 1, kiasi ambacho ni sawa na Sh. Mil. 250 kila mwaka. Watanzania wajitokeze kuungana nasi katika mbio hizi, ili kuokoa maisha ya wamama wanaoteseka na maradhi ya Fistula. Tuna mwezi mzima wa kujisajili na naamini tunaweza kufikia lengo kwa ushirikiano huu," alisema Zaipuna.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi, alisema taasisi yake inajisikia faraja kubwa kufanikisha utilianaji saini wa makubaliano hayo, sambamba na uzinduzi wa NMB Marathon 2021, huku akieleza kuwa mashindano hayo yana maana kubwa kwa maelfu ya kina mama wa Kitanzania.

"CCBRT ni wabobevu wa matibabu ya Fistula nchini, na tafiti zetu za awali zilionesha ukubwa wa tatizo miongoni mwa kinamama, lakini gharama kubwa za matibabu unakwamisha wengi wao kupata tiba za maradhi haya. 

"Ndio maana tunachukua nafasi hii kuwapongeza NMB kwa uamuzi wao wa dhati wa kuwabeba wamama wa Kitanzania takribani 60 watakaolipiwa Sh. Mil. 250 kila mwaka katika kipindi cha miaka minne. Kila Mtanzania anapaswa kuunga mkono jitihada hizi chanya kwa afya za kina mama," alisema Msangi.

NMB Marathon zitakuwa na kategori tatu za mbio za kilomita 21 (nusu marathon), kilomita 10 na kilomita 5, ambako washindi wa kwanza hadi wa 10 watapata medali na fedha taslimu.

Kwa mujibu wa Mratibu wa NMB Marathon 2021, David Marealle, ada ya kujisajili kushiriki mnio hizo ni Sh. 30,000 kwa kilomita 21 na Sh. 20,000 kwa mbio za kilomita 10 na kilomita 5.

Marealle aliongeza kuwa, washindi wa mbio za kilomita 21 wanaume na wanawake watajinyakulia Medali ya Dhahabu na fedha taslimu Sh. 1,400,000, huku washindi wa pili wakitarajiwa kutwaa Medali za Fedha na Sh. 1,100,000, wakati washindi wa tatu wakitengewa Sh. 700,000 na Medali za Shaba.

Zawadi za washindi wa kilomita 10 wanawake na wanaume ni: kinara medali ya dhahabu na Sh. 700,000, washindi wa pili medali za fedha na Sh. 500,000, huku washindi wa tatu wakitarajiwa kubeba medali za Shaba na Sh. 300. 

Katika mbio za kilomita 5, washindi upande wa wanawake na wanaume watajipoza na Medali za dhahabu na Sh. 250,000, washindi wa pili medali za fedha na Sh. 150,000, huku washindi wa tatu wakiambulia medali za shaba na Sh. 100,000 taslimu.


 

No comments:

Post a Comment

Pages