Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (katikati), Rais wa CAF Dkt. Patrice Motsepe (kushoto) na Waziri wa Habari, Innocent Bashungwa wakijadili mambo mbalimbali yanayohusu michezo. |
Na John Mapepele- WHUSM
Shirikisho
la Mpira wa Miguu wa Barani Afrika (CAF) limepongeza mikakati
inayofanywa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza
michezo hususan Soka, ambapo wiki ijayo atapokea kombe la CECAFA 2021 la
vijana wenye umri chini ya miaka 23.
Hayo
yameelezwa na Rais wa CAF, Dkt. Patrice Motsepe leo, Agosti 13, 2021
wakati alipokutana na Viongozi Wakuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Shirikisho la Soka nchini na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim
Majaliwa ambapo amesema timu ya taifa ya Tanzania ina uwezo wa kuwa timu
bingwa barani Afrika kutokana na umahiri iliyonayo sasa.
Aidha
ameipongeza Tanzania kuwa nchi ya kuigwa kutokana na wananchi wake
wengi kupenda michezo na hasa panapokuwa na mechi zinazowakutanisha
vilabu vikubwa nchini kwa vile zinawaleta mashabiki hata kutoka nchi
Jirani.
Ameisihi Serikali
kuwa na mpango madhubuti wa kupata maeneo ya kufanyia mazoezi, viwanja
bora na kuandaa vijana kuanzia umri mdogo, kuwa na taasisi za
Serikali na binafsi ya kufundisha soka, na makocha ili kuwa na
wachezaji wa kimataifa.
Kwa
upande wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Kassim Majaliwa
amesema Serikali imeanza kuboresha michezo nchini chini ya mpango
unaohusisha Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Rais
TAMISEMI na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambapo mpango
huo unalenga kuibua vipaji vya vijana kupitia mashindano ya UMITASHUMTA
na UMISSETA, Vyuo Vikuu na Vyuo vya kati
Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa ametaja
miongoni mwa jitihada zilizolivutia Shirikisho hilo zinachukuliwa na
Serikali katika kuendeleza michezo nchini kuwa ni pamoja na kuondolewa
VAT kwenye nyasi bandia ili kuboresha miundombinu ya michezo nchini,
kutunisha Mfuko wa Maendeleo ya Michezo unaosimamiwa na Baraza la
Michezo nchini (BMT) na mkakati wa kurudisha uhai wa michezo katika
Shule za Msingi (UMITASHUMTA) pamoja na Shule za Sekondari (UMISSETA).
Waziri Bashungwa
amemshukuru Mhe. Waziri Mkuu kwa kuongoza vizuri majadiliano baina ya
Serikali na Rais huyo wa CAF ambapo amefafanua kuwa Serikali imejipanga
vizuri kutumia michezo kama mkakati wa kuendeleza utalii nchini.
Akitolea mfano amesema katika Mkutano Mkuu wa CAF unatarajiwa kufanyika
nchini na kuwashirikisha Marais 54 wa Mpira katika nchi mbalimbali
Barani Afrika na ujumbe wao utaleta faida kwenye sekta ya utalii kwa
kuwa baada ya mkutano watapata fursa ya kutembelea Hifadhi za Taifa na
maeneo mengine ya yenye vivutio vya utalii hapa nchini.
Ujumbe
wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na michezo katika majadiliano
hayo uliongozwa na Waziri mwenye dhamana ya Wizara hiyo, Mhe. Innocent
Bashungwa, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Ally Possi na Rais wa Shirikisho la
Soka Nchini Tanzania Wallace Karia.
No comments:
Post a Comment