HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 14, 2021

Vijana ACT walilia ushirikishwaji mpango wa maendeleo ya Taifa


Viongozi wa Ngome ya Vijana ACT Wazalendo Mkoa wa Dar es Salaam wakizungumzia umuhimu wa Vijana kushirikishwa katika mipango ya Dira ya Maendeleo ya Taifa.

 

 Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Vijana nchini wameiomba Serikali kutowaacha nyuma katika utekelezaji wa Mpango wa Dira ya Maendeleo ya Taifa wa 2025 ili kujenga Taifa lililo bora.

Ushauri huo ulitolewa na Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Dar es Salaam, Ndugu Leonid Tairo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana duniani yaliyofanyika Makao makuu ya chama hicho Kijitonyama jijini Dar es Salaam Agosti 12,2021.

Alisema mpango wa Dira ya Maendeleo ya Taifa unaotarajia kufika kilele chake 2025 hauwezi kuwa na tija endapo vijana hawatashirikishwa ipasavyo katika nyanja mbalimbali.

Mbali na hilo, Mwenyekiti huyo alisema uandikaji wa Katiba mpya Tanzania ni moja ya takwa la msingi kwa vijana kwani itawahakikishia fursa mbalimbali kuanzia kizazi cha sasa na kijacho.

Tairo alisema ni jukumu la vijana kushikamana kuhakikisha Taifa linapata Katiba mpya pamoja na Tume huru ya Uchaguzi kwa kushirikiana na makundi mengine ya kijamii, zikiwamo asasi za kiraia, taasisi za dini na makundi mengine yanayopigania upatikanaji wa Katiba mpya na Tume ya Uchaguzi iliyoridhiwa na Watanzania.

"Sisi vijana wa Dar es Salaam tunapendekeza kwa Serikali ishirikishe vijana katika upangaji, utekelezaji, usimamizi na tathmini mbalimbali ya maendeleo katika jamii.

"Hivi sasa robo tatu ya vijana nchini wamejiajiri katika sekta isiyokuwa rasmi wakiwamo wale wanaomaliza vyuo mbalimbali bila kuwa na uhakika wa ajira wala mitaji ya kuwaeezesha kujiajiri jambo ambalo linahitaji kuangaliwa kwa jicho la pekee na kupatiwa suluhisho la kudumu"alisema.

Katika hatua nyingine, Tairo aliwataka vijana nchini kujenga utamaduni wa kushiriki shughuli za maendeleo sambamba na kuhudhuria vikao vya kijamii katika maeneo yao pamoja na kipenda kujisomea vitabu na maandiko mbalimbali ili kujenga uelewa kwa mambo mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

Pages