HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 01, 2021

Kipanga avitaka vyuo kuongeza udahili

 

Baadhi ya wanafunzi wakifanya udahili katika viwanja vya Mnazi Mmoja katika Maonesho ya Vyuo Vikuu.

 


NAIBU Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga (katikati), akiongozana na Mwenyekiti wa TCU, Prof. Charles Mgone (kushoto) na Katibu Mtendaji wa TCU, Prof. Charles Kihampa, wakitembelea mabanda katika Maonesho ya 16 ya Elimu ya Sayansi na Teknolojia yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam.

 

Na Selemani Msuya

NAIBU Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga amesema ili Tanzania iweze kufikia uchumi wa kati na wajuu inapaswa kuwa na rasilimali watu wenye elimu ya juu kwa asilimia 12 na elimu ya kati asilimia 26.

Kipanga alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati akifunga monesho ya 16 ya vyuo vikuu ambayo yanaratibu na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Ilala, jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri alisema katika maonesho hayo ambayo yalikuwa na kauli mbiu isemayo ‘Tuendelee kukuza na kudumisha uchumi wa kati kupitia elimu ya juu, sayansi na teknolojia’ hivyo itakuwa vizuri kauli ichochee udahili ili kupata wahitimu ambao watachangia kufikia uchumi wa kati.

Alisema kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2016 zinaonesha watu wenye ujuzi wa elimu ya juu nchini ni asilimia 3.3 huku ujuzi wa kati ukiwa ni asilimia 17 hivyo amevitaka vyuo kuongeza jitihada za kufikia asilimia 12 na 26 ambazo zinahitajika.

Naibu Waziri Kipanga alisema ili kufikia uchumi wa kati wa juu ifikapo 2025/2026 vyuo vinapaswa kuwekeza katika elimu hasa kwenye eneo la sayansi ili kuchochea uzalishaji.

“Hii inaonesha kwamba nado taasisi zetu za elimu ya juu zinawajibu wa kuongeza udahili wa wanafunzi ili waweze kuja kutumikia nchi kwenye sekta mbalimbali.

Kwa sasa takwimu zinaonesha ushiriki wa wanafunzi katika elimu ya juu ni asilimia 6.1 huku katika nchi za Jangwa la Sahara ikiwa ni asilmia 9.4 na Kenya ni asilimia 11,” alisema.

Kipanga alisema pamoja na changamoto hiyo ya uchache wa wasomi wa elimu ya juu kitakwimu lakini katika miaka mitano kumekuwepo na mafanikio ambapo Serikali imeendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wengi kwa miaka mitano iliyopita.

Aidha, alisema wameendelea kuboresha miundombinu na mazingira ya kufundishia katika vyuo vikuu hivyo ni imani yao kuwa hilo litachangia kutoa wahitimu wenye uwezo wa kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.

“Tumetoa mikopo kwa wanafunzi 149,506 kwa mwaka 2020 kutoka wanafunzi 125,126 mwaka 2015 na mengine mengi ambayo yanandelea kuboresha elimu nchini.

Naye Makamu Mwenyekiti TCU, Profesa Charles Mgone alisema maonesho hayo yamekuwa na mafanikio makubwa mwaka hadi mwaka jambo ambalo linawapa faraja.

Prof. Mgone alisema TCU imejipanga kuwa taasisi imara, kitaifa, kikanda na kimataifa ili kuhakikisha elimu ya Tanzania inakuwa bora na yenye ushindani.

No comments:

Post a Comment

Pages