HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 14, 2021

KUWALINDA WATOTO NI JUKUMU LETU-DK. JINGU

 


Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu (kulia) akiwasikiliza Watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani katika Kituo cha Babawatoto kilichopo Mburahati, Wilaya ya Ubungo, mkoa wa Dar es Salaam.

 

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Baadhi ya wamiliki wa mabasi wametajwa kuchangia ongezeko la watoto waoishi na kufanya kazi mitaani.

Hali hiyo imebainika wakati Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu alipotembelea vituo vya kuhudumia watoto hao ambao wamemueleza wanavyosafiri kutoka mikoani kwenda jijini Dar es Salaam kwa nauli pungufu.

"Lazima tuongee na LATRA ili tuweze kukaa na wenye mabasi ili kuliweka sawa suala hili, haiwezekani mtoto mdogo hana mtu anayeambatana naye unampakia, ni jukumu letu wote kuwalinda bila kujali ni wako au siyo wako" alisema Jingu.

Dkt. Jingu pia ametoa wito kwa mashirika mengine yote yanayofanya kazi ya kuwasaidia watoto hao kuhakikisha wanawarekebisha na kuwarudisha nyumbani kwao mapema.

Aidha, amewataka kwa watoto wanaoshindikana kurudi makwao, wapelekwe kwenye makao ya watoto ya Serikali.

Naye Mkurugenzi wa Kituo hicho Mgunga Mwamnyenyelwa amesema kilianza mwaka 2017 na hadi sasa wameshafikia watoto na vijana zaidi ya 2,500 kwa namna mbalimbali ikiwemo kuwarudisha nyumbani watoto 275 huku vijana 320 wakipatiwa ujuzi mbalimbali ili waweze kujitegemea.

Awali akiwasilisha taarifa ya utoaji wa huduma za shirika hilo, Meneja mradi wa kituo Johnson Mtango amesema kutokana na jitihada wanazofanya za kuwatoa watoto mitaani na kuwapatia huduma, inaonesha tatizo kupungua kwani utafiti uliofanywa mwaka 2017 na 2021 kulikuwa na watoto 2,504 mitaani lakini sasa hivi watoto ni 1,504 kwa mkoa wa Dar es salaam pekee.

Amesema hata hivyo changamoto bado ipo kwani kuna ongezeko la watoto wapya kila siku kuingia mjini wakitokea mikoani na kupitia vituo vya mabasi hususani Kituo kikuu cha Mbezi na  Mbagala Rangi Tatu.

"Sababu za watoto kukimbilia mijini ni kukosa malezi bora, umasikini na ushawishi wa wenzao, inaonesha tatizo limepungua lakini bado Kuna changamoto ya watoto wapya kuja mitaani." aliongeza Mtango.

No comments:

Post a Comment

Pages