Mstahiki Meya wa Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera Godson Gypson akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani kilicholenga kujadili taarifa mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kata.
Na Lydia Lugakila, Bukoba
Mstahiki Meya Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera, Godson Gypson, ameagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani Bukoba kuanza msako wa majambazi wanaovamia kuteka na kuwaua wananchi katika eneo la Kyakairabwa kata Nyanga.
Mstahiki meya ametoa kauli hiyo katika kikao cha baraza la madiwani kilicholenga kujadili taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya kata kilichofanyika katika uwanja wa Kaitaba.
Kauli ya mstahiki Meya imekuja kufuatia diwani wa kata ya Nyanga Stephen Mutashubilwa Ngaiza kupokea kilio cha wananchi wa eneo hilo waliogubikwa na vitendo vya mauaji na unyanganyi vinavyoendelea kutikisa katika eneo linalotokea kinapojengwa kituo cha mabasi cha Kyakairabwa kuelekea Nyarubanja eneo linalotajwa kuwa pori.
"Mh, Mstahiki meya nimetumwa na wananchi wa eneo hilo ambalo limechukua maisha ya watu, wanaomba serikali walau ibadilishe eneo hilo kuwa matumizi ya ardhi kutoka pori kuwa makazi ya watu ili kuwanusuru wananchi hao dhidi ya majanga hayo kwani ndani ya mwezi mei mwaka 2021 majambazi katika eneo hilo wamemvamia kijana ambaye ni ndugu yangu akiwa na pikipiki wamemkata kata mapanga Kisha kumnyofoa macho" alisema diwani wa kata ya Nyanga.
Akijibu janga hilo mstahiki meya ameagiza kamati ya ulinzi na usalama wilayani Bukoba kuanza kuwasaka mara moja majambazi hao ambao wamekuwa wakifanya unyama huo huku akitaka kupewa majibu ya haraka juu ya kwanini wananchi hao wamekuwa wakivamiwa bila hatua madhubuti kuchukuliwa dhidi yao.
"OCD, kamati ya ulinzi na usalama fanyia kazi haraka suala hili na kunipa majibu ya haraka ya kwanini wananchi wanauwawa na msako uanze mara moja afisa ardhi na mkurugenzi hakikisha kama meneo hayo ni pori na hakuna mpango wowote wa maendeleo badilisha matumizi ya viwanja hivyo kuwa makazi acheni kutunza vichaka." tunataka wananchi waishi kwa amani alisema mstahiki meya huyo.
Kwa mujibu wa diwani wa kata ya Nyanga Mutashubilwa eneo hilo limekuwa ni changamoto sana kwani kuanzia muda wa saa moja usiku hali uanza kuwa mbaya jambo linalowapelekea wakazi hao kupita umbali mrefu ili kuepukana na hali hiyo.
Aidha ameongeza kuwa serikali iliyopita kwa miaka ya 20 ilitenga eneo hilo lenye muonekano wa hifadhi kwa ajili ya ujenzi wa viwanda lakini halikutumika kwa shughuli hiyo.
Hata hivyo akizungumzia janga hilo kwa niaba ya mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba Dr waziri Msafiri amesema matukio hayo yanatakiwa kushughulikiwa na mamlaka husika ikiwemo kufuatilia suala hilo ili kuona hali ya usalama inaimalishwa katika eneo hilo.
No comments:
Post a Comment