HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 20, 2021

KWAHERI MWALIMU KASHASHA

 

Marehemu Alex Kashasha.

 

ADELADIUS MAKWEGA, WHUSM-DODOMA

 

Mchezaji soka, mchambuzi wa soka, mwalimu wa michezo, mkufunzi wa vyuo vya ualimu Alex Gashasha (Mwalimu Gashasha) amefariki dunia. Walio wengi haswa wapenzi wa kabumbu nchini Tanzania na Afrika ya Mashariki jina hilo si geni bali lipo masikioni na machoni mwao haswa mechi za kabumbu zinapopigwa uwanjani, ziwe za kitaifa ama kimataifa.

 

“Ni kweli bao hili limefungwa kiufundi zaidi, haswa kwa kutumia mtindo 4,4,2..” ndivyo alivyokuwa akiongea kwa kutumia ujuzi wake wa ualimu wa michezo aliosomea miaka ya themanini na kuchambua michezo wa soka ambapo hapo awali lilikuwa jambo geni nchini Tanzania.

 

Kumfahamu Mwalimu Ghashasha niliifunga safari ya kifikra mpaka mwaka wa 2014 ambapo mimi binafsi niliweza kumuona kwa mara ya kwanza wakati wa kombe la dunia na mimi nikiwa mtangazaji na mtayarishaji vipindi wa TBC Taifa.

Ninachoweza kukumbuka ni kuwa mtangazaji aliyekuwa naye karibu sana alikuwa ni Jesse John kwani ndiye alikuwa mtayarishaji na mtangazaji wa soka tangu Kombe la Dunia la mwaka 2010, enzi zile za TBC chini ya Mkurugenzi Tido Mhando.

 

“Ni kweli mimi ndiye niliyeweza kuhakikisha mwalimu Gashasha anakuja TBC Taifa na kila wakati kulipokuwa na mechi ya kabumbu aliweza kupata nafasi ya kuwepo uwanjani  kwa mechi za nyumbani na hata studioni kwa mechi za kimataifa kuchambua mechi husika.” Anasema Jesse John.

 

Kabla ya kuja TBC nikiwa katika harakati mbalimbali za maisha Jesse John anasema alikutana na Mwalimu  Gashasha mwaka 1988 akiwa mkurufunzi wa mafunzo ya Ualimu wa Daraja A Chuo Cha Ualimu Butimba. Wakati huo huo Mwalimu Gashasha alikuja kujiendeleza katika Ualimu wa Michezo akitokea kazini maana yake alikuja katika mafunzo kazini.

 

Kwa wakati huo Waziri Mkuu wa sasa Kassimu Majaliwa alikuwa miongoni mwa wakurufunzi waliokuja kujifunza ualimu huo wa michezo anasema Jesse John.

 

“Tukiwa Chuoni Mwalimu Gashasha alikuwa akicheza mpira huku akiwa  kocha wetu, mimi (Jesse Johni) nikiwa golikipa wa timu ya Chuo cha Ualimu Butimba, Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa akiwa mchezaji nambari saba.” Anaongeza Jesse John.

 

Maisha yana safari ndefu sana nilikutana na mwalimu Gashasha tena Kombe la Dunia la mwaka 2014 akiwa mkufunzi wa Chuo cha Ualimu Vikundu Mkoa Pwani na kwa kuwa nilikuwa namfahamu kama mwalimu wa michezo na mtu anayeifahamu michezo kitaalamu sikuwa na ajizi ndipo akaja TBC tukaanza kuchambua michezo katika redio yaani TBC Taifa.

 

“Wadau wengi wa mpira wamejifunza soka kupitia kwake kwani wakati anachambua mpira wengine walikuwa wakiandika kutokana na uchambuzi wake na alikuwa hachambui  kwa kusoma katika mitandao bali aliusoma na kuucheza huo mpira wa miguu.” Alisisitiza Jesse John.

 

Mwalimu Gashasha aliucheza mpira wa miguu akiwa shuleni, chuo cha Ualimu Butimba na  aliweza kufundisha mpira wa miguu katika timu mbalimbali kwa mfano Majimaji ya Songea kwa kipindi kifupi, timu ya Maji Mara, timu ya Mkoa wa Mara wakati wa mashindano ya Taifa CUP. Kwa hakika kifo chake ni msiba mkubwa kwangu mie na wadau wengine wa soka.

 

“Mara ya mwisho kuonana naye ilikuwa ni saa 9 alasiri Agosti 18, 2021 alikuwa akiniuliza juu ya usajiri wa timu za Simba na Yanga, huku akiniandikia yale tuliyokuwa tunazungumza katika karatasi. Alikuwa akizungumza kwa tabu sana.” Alieleza Jesse John.

 

“Wapenzi wa mpira miguu wanajua kuwa mpira huu ulikuwa na vionjo kupitia kwa uchambuzi wa Mwalimu Ghashasha, watu waliokuwa wakitazama Runinga lakini cha kushangaza walikuwa wakitumia sauti ya matangazo ya TBC Taifa kupata utamu na vionjo vya uchambuzi wa mwalimu Ghashasha.” Aliongeza Mtangazaji Jesse John.

 

Mwalimu Alex Ghashasha ameacha Mjane na watoto mabinti wawili. Raha ya milele umpe ee Bwana na mwanga milele umwangazie, apumzike kwa amani, amina.

 

 

No comments:

Post a Comment

Pages