HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 13, 2021

MRADI WA RAFIC KUONGEZA UDAHILI DIT


Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano na Viwanda Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Dk. John Msumba akielezea Mradi wa RAFIC utakavyosaidia kuongeza udahili wa wanafunzi wasichana shuleni hapo.


Na Mwandishi Wetu

 
KATIKA kuhamasisha wanafunzi wasichama kusoma masomo ya sayansi hadi ngazi ya chuo kikuu, Taasisi ya Teknlojia Dar es Salaam (DIT), kupitia mradi wa Kituo cha Umahiri cha Tehama (RAFIC) imeanza kuhamasisha wasichana kupenda masomo ya sayansi na hatimaye kujiunga na DIT.
 
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano na Viwanda DIT, Dk. John Msumba wakati akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara ya mafunzo kwa wanafunzi wasichana kutoka shule mbalimbali za sekondari za mkoa wa Dar es Salaam.
 
Dk. Msumba alisema kwa muda sasa uwiano kati ya wanafunzi wasichana na wavulana katika vyuo vya sayansi na ufundi ni mdogo hivyo wanaamini kupitia Mradi wa RAFIC wanafunzi wasichana watasoma masomo ya sayansi.
 
“Tumewaleta wanafunzi wasichana kuja kuona namna dada zao wanaosoma DIT wanavyobuni vitu vingi jambo ambalo linathibitisha kuwa masomo ya sayansi sio magumu kama ambavyo inasemwa,” alisema.
 
Alisema DIT imepewa nafasi ya kuwa na kituo hicho cha Kanda kwa Afrika Mashariki, moja ya mkakati ni kujenga hosteli ya wasichana.
 
Mhadhiri huyo mwandamizi alisema pia wamejipanga kutekeleza mradi huo kwa kufanya kazi na viwanda ili kuhakikisha ongozeko hilo la wahitimu wa masomo ya sayansi wanakuwa na mchango kwenye maendeleo ya nchi.
 
Dk Msumba alisema Tanzania imepata nafasi ya kupata miradi minne ambapo 
ambapo taasisi ya DIT ni moja wapo.
 
“Sisi DIT tunanzisha Kituo Mahiri kwenye Uchakataji wa Ngozi na RAFIC itakayojikita katika masuala ya TEHAMA,” alisema.
 
Mhadhiri huyo alisema mradi huo unatarajiwa kufikia ukomo mwaka 2024 hivyo kuwataka wanafunzi wakike kusoma masomo ya sayansi ili kuwepo na uwiano mzuri wa makundi hayo.
 
Kwa upande wake Mratibu wa Kitengo Mambo ya Jinsia na Mhadhiri wa Umeme na Mawasiliano Chuo cha DIT, Nsantule Nzowa alisema Mradi wa RAFIC ni fursa muhimu ya kuchochea ongezeko la wanafunzi wakike kuanzia ngazi ya chini.
 
Nzowa aliwataka wanafunzi wa sayansi kutoka Sekondari mbalimbali kutumia Mradi wa RAFIC kuhakikisha wanafikia malengo yao.
 
Mhadhiri huyo alisema serikali, wazazi na jamii wanapaswa kuhamasisha wasichana kusoma masomo ya sayansi kuanzia ngazi ya chini ili kuwa na kundi kubwa litakalonufaika na RAFIC.
 
Mwalimu Reginald Komunyo wa Sekondari ya Debrabant, alisema ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwani imeonesha wasichana wanaweza wakipewa nafasi.
 
Alisema iwapo masomo ya sayansi yatapewa kipaumbele miaka michache ijayo Tanzania itafika uchumi wa kati na viwanda ambavyo vitaendeshwa na Watanzania wenyewe.
 
Naye Mwanafunzi, Mwamini Mohammed kutoka Sekondari ya Makongo aliiomba Serikali kuwekeza katika masomo ya sayansi kwa kuwa yanachochea ubunifu ambao utachangia kutatua changamoto za sekta mbalimbali.
 
“Nimeona mambo mengi ya ubunifu ambayo yamefanywa na dada zangu naamini hata mimi kama ningepata mwanzo mzuri ningekuwa mwanasayansi, ila nimechelewa na kuchagua masomo ya sanaa,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages