Marehemu Mwalimu Alex Theoganis Kashasha.
DAR ES SALAAM, TANZANIA
MWILI wa aliyekuwa mchambuzi mahiri wa soka nchini, Mwalimu Alex Theoganis Kashasha, unatarajiwa kuzikwa Jumatatu Agosti 23, kwenye makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Mwalimu Kashasha aliyepata umaarufu Mkubwa kutokana na aina yake ya uchambuzi wa soka, uliojaa ufundi na mbinu, alifariki Dunia Alhamisi Agosti 19, kwenye Hospitali ya Kairuki, mikocheni, jijini Dar es Salaam, alikokuwa akipatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Familia, Mzee Deus Kashasha, mwili wa marehemu utafanyiwa ibada kesho Jumapili kuanzia saa 4 asubuhi, kwenye Kanisa la Ufunuo, lililopo Buza Kipera wilayani Temeke, kabla ya mwili kurejeshwa nyumbani kwa marehemu kusubiri ibada na maziko Jumatatu mchana.
"Kesho Jumapili kutakuwa na ibada na kutoa heshima za mwisho katika Kanisa la Ufunuo, hapa Buza Kipera, ambayo tunaamini itakuwa ndefu kidogo kutokana na dhehebu lake, kisha mwili utarudi na kulala hapa. Jumatatu tutakuwa na hutoaji heshima kwa ndugu na waombolezaji, Kisha ibada ya maziko na kumaliza taratibu kwa kumzika katika makaburi ya Kinondoni," alisema Mzee Kashasha.
Hadi umauti unamkuta, Mwalimu Kashasha alikuwa akifanyakazi katika Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), alikokuwa akifanya uchambuzi wake wa soka katika vyombo vya habari vya shirika hilo, ikiwemo TBC FM, TBC Taifa na Televisheni ya TBC1.
No comments:
Post a Comment