HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 24, 2021

NIT kushirikiana na NAS Tanzania


Mkuu wa Chuo cha Taifa Cha Usafirishaji (NIT) Profesa Zacharia Mganilwa (wa pili kutoka kushoto) na Meneja Mkuu wa NAS Dar Airco Tanzania Miguel Serra (wa pili kutoka kushoto) walionyesha mikataba waliyosaini pamoja mbele ya mjumbe wa bodi ya NAS Afrika Prof. Costa Ricky Mahalu (wa kwanza kulia) jijini Dar es Salaam Mwishoni mwa wiki.

 

Na Suleiman Msuya


CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), kimesaini mkataba wa ushirikiano na National Aviation Service (NAS) Dar Airco Tanzania katika mipango chanya ambayo itawasaidia wanafunzi wa mafunzo ya anga na lojistiki katika usafirishaji kupata mafunzo kwa njia ya vitendo.

NAS ilianza shughuli zake nchini Kuwait mnamo mwaka 2003 na kuingia rasmi nchini Tanzania mwaka 2016, imebobea katika utoaji wa huduma mbalimbali kwenye zaidi ya viwanja vya ndege hamsini (50) Ulimwenguni kote.

Mkataba wa makubaliano ulisainiwa mwishoni wa wiki iliyopita katika Kampasi ya chuo hicho Mabibo, jijini Dar es Salaam baina ya Mkuu wa Chuo Profesa Zacharia Mganilwa na Meneja Mkuu wa NAS Dar Airco Tanzania Miguel Serra mbele ya mjumbe wa bodi ya NAS Afrika Prof. Costa Ricky Mahalu.

Akiongea muda mfupi kabla ya hafla ya utiaji saini, Prof Mahalu alisema: 
 
"Makubaliano haya yanakusudia kuanzisha ushirikiano kati ya NAS na NIT katika kusaidia wanafunzi wetu kupata mafunzo kwa vitendo."

Prof Mahalu ameongeza: "Programu ambazo zinatolewa NIT zinakwenda kukifanya chuo hiki kuwa taasisi bora kabisa katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na barani Afrika kwa ujumla."

"Kwa hivyo, NAS Tanzania katika makubaliano haya itatoa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya anga na lojistiki na usafirishaji kwa kuhakikisha kuwa wanapata mafunzo bora ambayo yatasaidia kufanya kazi nje ya nchi," alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo NIT, Profesa Mganilwa alisema: "Makubaliano haya yatatoa  fursa kwa wanafunzi ambao wanasoma kozi za anga,lojistiki na usafirishaji kupata nafasi ya mafunzo kwa vitendo.

Prof Mganilwa ameongeza: "Ushirikiano huu utaboresha na kuiimarisha Shule kuu ya Usafiri wa Anga na Teknolojia ya NIT kutoa wataalamu zaidi ambao watasaidia nchi katika sekta ya anga."

Makubaliano haya yataimarisha mafunzo ya Usafiri wa anga, lojistiki na usafirishaji chuoni hapo ambapo hivi karibuni Taasisi hiyo ilipata dola za kimarekani milioni 21.25 kutoka Benki ya Dunia ikilenga kuboresha mafunzo ya anga.

Alisema kupitia shule ya kuu ya Teknolojia ya Usafiri wa Anga iliyopo chuoni hapo wameanza kutoa mafunzo ya usafiri wa anga ya ubobezi ambapo mipango ni kuzalisha wataalamu wengi ambao watasaidia uendeshaji katika sekta ya anga nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja Mkuu wa NAS Dar Airco Tanzania Serra alisema: "NAS Tanzania inafurahi kuingia katika makubaliano haya na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji ili kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi."

Meneja Mkuu aliongeza kuwa wanafunzi wa NIT watapata uzoefu wa kimataifa na wakati huo huo kupata nafasi za ajira katika ofisi zao zilizopo katika nchi zaidi ya 20 Duniani.

"Mbali na kupata nafasi ya mafunzo kwa vitendo, wanafunzi watapata nafasi ya kuajiriwa na ofisi zetu ambazo sasa ziko katika nchi  20 duniani na zaidi ya viwanja vya ndege 50 ulimwenguni," alisema.

Serikali imeamua kuwekeza zaidi katika Chuo hicho ili kuboresha mafunzo ikiwa ni pamoja na kuweza kutoa wahitimu bora watakaoleta tija kwenye sekta ya usafirishaji ikiwemo sekta ndogo ya usafiri wa anga ambayo inakua kwa wastani wa asilimia 12 kwa mwaka.


No comments:

Post a Comment

Pages