HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 24, 2021

VIJANA WATAKIWA KUTUMIA FURSA ZINAZOWEKWA NA SERIKALI

 
Mwakilishi wa jimbo la Pangawe, Ali Suleiman Mrembo amewaasa vijana kuzitumia fursa zinazowekwa na serikali pamoja na taasisi zao katika kujiendeleza kiuchumi.


Akizungumza Kongamano la wanawake na vijana lililofanyika kwenye ukumbi wa Sanaa Rahaleo, Mrembo amesema serikali kupitia mfuko wa uwezeshaji na ufadhili kupitia Taasisi ya Khalifa Fund inawapatia vijana rasilimali na mitaji ya kuwawezesha kujiajiri

Aidha amesema kuna fursa mbali mbali kupitia sekta ya utalii, uvuvi na kilimo ambazo vijana bado hawajazitumia ipasavyo.

Kwa upande wake Naibu Katibu wa Jumuiya hiyo iliyoanzishwa mwaka 2017 Bi Raya Hamad Mchere amesema wamelenga kuleta mabadiliko kwa vijana kwa kuwapatia stadi na taaluma za maisha kwa kushirikiana na Serikani pamoja na wahisani ili vijana na wanawake wafikie malengo ikiwemo kujiajiri wenyewe

Nao washiriki wa kongamano hilo lililoandaliwa na Jumuiya ya Maendeleo ya Wanawake na Vijana, wameishukuru BIWO na kuziomba taasisi mbali mbali kuendelea kutoa elimu juu ya upatikanaji wa masoko na ujasiriamali katika sekta mbali mbali ili kujiimarisha kiuchumi

Akifunga kongamano hiyo Mrajis wa Jumuiya zisizo za kiserikali Bw. Ahmed Khalid Abdulla amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa Jumuiya hizo ili ziweze kutekeleza shughuli zao kwa ufanisi.

Amesifu Jumuiya ya BIWO na kusema kuwa imefanya kazi kubwa ya kuwaandaa vijana kwa kuwapatia taaluma mbali mbali na kuwawezesha kutumia fursa zao kwa muda sahihi pamoja na kushiriki kwao katika masuala mbali mbali ya kimaendeleo 

Amefahamisha kuwa Serikali itahakikisha Wizara ya Uchumi wa Buluu inatoa taaluma kwa vijana kuzifikia fursa, kuwaandalia mazingira mazuri kwa wanawake na vijana ili kuendana na sera ya nchi kuelekea uchumi wa buluu

Ameongeza kuwa hatua hiyo ni chachu ya kujipatia ajira kwa vijana na kukuza uchumi ambapo ameahidi kuwapatia BIWO printa mbili kwa ajili ya shughuli za kiofisi 

Jumla ya mada nne zimewasilishwa katika kongamano hilo zikiwemo Vijana fursa na wakati iliyowasilishwa na Mwl. Hassan Ibrahim Suleiman, matumizi sahihi ya mawasiliano ya mitandao iliwasilishwa na wataalamu kutoka TCRA, nafasi ya vijana katika vyombo vya maamuzi iliyowasilishwa na Mhe Hudhaima Mbarouk Tahir mwakilishi wa Vijana na Mada ya nne ni maendeleo ya Uchumi wa Buluu iliyotolewa na ndg Shaaban Hassan Ramadhan kutoka Idara ya Uratibu na Maendeleo ya Uchumi wa Buluu.


No comments:

Post a Comment

Pages