HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 22, 2021

Rais Samia aipongeza Azam Media kwa uwekezaji Sekta ya Michezo

DAR ES SALAAM, TANZANIA


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameipongeza Kampuni ya Azam Media, inayomiliki vituo vya Televisheni vya Azam TV kwa uwekezaji mkubwa kwenye Sekta ya Michezo nchini, huku akiwataka wadau zaidi kujitoa kufuata nyayo zao, kwani Michezo ni Biashara kubwa kwa sasa duniani.

Rais Samia ameyasema hayo Ikulu jijini Dar es Salaam leo Jumapili Agosti 22, wakati akipokea taji la Michuano ya Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati (U-23 CECAFA Challenge Cup 2021), lililotwaliwa na timu ya Taifa ya Tanzania kwa vijana wenye umri chini ya miaka 23 katika fainali nchini Ethiopia, walikoichapa Burundi kwa penalti 6-5 baadabya sare tasa.

Kikosi hicho, ambacho kilikuwa chini ya Kocha Mkuu Kim Poulsen, kilialikwa Ikulu kukabidhi taji hilo kwa Rais Samia, ambaye aliwapongeza wapambanaji hao, lakini akaenda mbali kwa kuwamwagia sifa Azam Media, kutokana na uwekezaji mkubwa inaofanya katika michezo nchini, ilikosaini kandarasi ya miaka 10 ya Haki za Matangazo ya Televisheni kwa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL), huku ikiamsha ari ya marejeo ya mchezo wa masumbwi, ambao alikiri kuwa havutiwi na matokeo yake yanayoambatana na kuumizana kwa mabondia.

"Nitoe wito kwa taasisi na Kampuni mbalimbali za kitaifa na kimataifa, kutuunga mkono katika uwekezaji michezoni, hasa ukizingatia hii ni biashara kubwa duniani kwa sasa. Na hapa niipongeze sana Kampuni ya Azam. Wamejitokeza vizuri kwenye Michezo. Wamejitokeza kwenye mpira wa miguu, lakini pia kwa sasa wako katika 'vitasa,' mchezo ambao mimi siupendi kabisa, mtu akipigwa huko mi naumia.

"Lakini ujio wao katika ngumi umeleta hamasa kubwa mitaani, ukipota huko, unaona watu wakitambia matokeo.. Kampuni ziige mfano wa Azam kuendeleza michezo nchini. Kwa wazazi wito wangu kwao Ni kutowakatisha tamaa vijana wao, wawasapoti katika michezo, tuwaruhusu kwa uwingi kushiriki michezo ili kukuza ajira na kuleta amani na utulivu kuanzia ngazi ya familia na Taifa," amesema Rais Samia katika hafla hiyo.

Kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan imekuja takribani mwezi mmoja tu tangu Azam Media iliposaini mkataba mnono wa Haki za Matangazo ya Televisheni (TV Rights), wenye thamani ya Bilioni 225.6, ambako kuanzia msimu ujao   kwa pamoja klabu zote zitapewa Sh. bilioni 8.8, huku bingwa wa Ligi Kuu akipewa bonasi ya Sh. Mil. 500, mshindi wa Pili Sh. Mil. 250, mshindi wa tatu Sh. Mil. 225 na mshindi wa nne Sh. Mil. 200.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akipokea Kombe la Ubingwa wa Mashindano ya Afrika Mashariki na Kati CECAFA U23 kutoka kwa Nahodha msaidizi wa Timu ya Taifa ya Vijana U23 Reliant Lusajo leo tarehe 22 Agosti, 2021 Ikulu Jijini Dar es Salaam. 
 
  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali wa michezo, Wachezaji wa Timu ya Taifa ya Vijana U23, Wanariadha walioshiriki michezo ya Olimpiki (Japan) mara baada ya kupokea Kombe la Ubingwa wa Mashindano ya Afrika Mashariki na Kati CECAFA U23 leo tarehe 22 Agosti, 2021 Ikulu Jijini Dar es Salaam. 


Baadhi ya Wachezaji wa timu ya Taifa ya Vijana U23 wakiwa katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya Pamoja na Wachezaji wa Timu ya Taifa ya Vijana ya U23 mara baada ya kukabidhiwa kombe la Ubingwa wa CECAFA U23 Challenge Cup leo tarehe 22 Agosti, 2021 Ikulu Jijini Dar es Salaam. Wengine katika picha ni Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa pamoja na  Rais wa TFF Wallace Karia.

 

Wachezaji wa Timu ya Taifa ya U23 wakiwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam leo tarehe 22 Agosti, 2021. PICHA NA IKULU.

No comments:

Post a Comment

Pages