Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Serikali imesema kuwa itasimamia sheria na
taratibu iliyojiwekea kwenye usimamizi wa mazao mbalimbali ikiwemo miwa, hivyo
haitatoa kibali kwa wafanyabiashara wa sukari badala yake kibali kitatolewa kwa
wazalishaji wa ndani kama kutakuwa na uhitaji.
Imebainisha kuwa kwa sasa nchini kuna ziada ya
Tani Zaidi ya 70,000 za sukari hivyo serikali haiwezi kutoa kibali chochote cha
uagizaji wa sukari nje ya nchi wakati uzalishaji unaendelea nchini.
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda ametoa
kauli hiyo ya serikali leo tarehe 16 Agosti 2021 mara baada ya kumalizika kwa
kikao cha kazi na wazalishaji wakubwa wa sukari hapa nchini kilichofanyika
katika ukumbi wa Wizara ya Kilimo Maarufu “Kilimo IV” Jijini Dodoma.
Amesema kuwa serikali kuendelea kutoa kibali
kuagiza sukari nje ya nchi sio sahihi kwani inahatarisha uzalishaji wa sukari
nchini jambo linalowakosesha ajira watanzania wengi huku likiwakosesha soko la
miwa kwa wakulima ambao miwa yao huchomwa kutokana na uwezo mdogo wa viwanda
vya ndani.
“Ninawaomba sana wafanyabiashara wote nchini watambue kuwa
serikali inapenda sana wapate faida kwenye biashara zao lakini hii ya sukari
waache tupambane ili tuweze kuzalisha ndani ya nchi” Amekaririwa Waziri Mkenda
Kauli hiyo ya Waziri wa Kilimo inajili wakati ambapo imebainika
kuwa kumekuwa na barua nyingi zinazowasilishwa Bodi ya Sukari kwa ajili ya
maombi ya kibali cha kuagiza sukari nje ya nchi.
“Mimi ndio msimamizi wa sheria kwahiyo msimuhangaishe sana
Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania kwamba yeye anakataa kuwapa ruhusa ya
kuingiza sukari, sheria haimruhusu na wala hainiruhusu mimi kutoa kibali hicho”
Mhe Mkenda
Sheria hiyo imeilekeza Wizara ya Kilimo kuhakikisha kuwa sukari
iingizwe kwa utaratibu ili kuwekeza Zaidi nchini, hivyo sheria hiyo haitabadilishwa
kama watu wanavyofikiri.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha wazalishaji wa sukari
Tanzania (TSPA) Ndg Seif Ally Seif amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kusimamia uimarishaji wa viwanda
nchini.
Amesema kuwa Uwekezaji wa sukari ni wa muda mrefu hivyo serikali
imeendelea kutoa hamasa kwa wawekezaji wa ndani na wa nje katika uwekezaji wa
viwanda mbalimbali ikiwemo vya sukari
MWISHO
No comments:
Post a Comment