Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam na Zanzibar, Donatus Richard,
akizungumza wakati wa uzinduzi wa Tamasha la Vyakula na Rasirimali za
Baharini (Zanzibar Sea Food Festival
2021), uliofanyika leo Septemba 8, 2021 jijini Zanzibar jana. Benki ya NMB ni wadhamini
wakuu wa tamasha hilo litakalofanyika Oktoba 8-9. Kushoto ni Mkuu wa
Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud na kulia ni Meneja
Msimamizi wa Biashara NMB Zanzibar, Abdallah Duchi. (Na Mpiga Picha
Wetu).
Mkuu wa
Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud (kushoto) akionesha eneo litakalofanyika Tamasha la Vyakula na Rasirimali za
Baharini (Zanzibar Sea Food Festival
2021), wakati wa uzinduzi wa tamasha hilo litakalofanyika Oktoba 8-9. Wa pili kushoto ni Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam na Zanzibar, Donatus Richard na wa pili kulia ni Meneja
Msimamizi wa Biashara NMB Zanzibar, Abdallah Duchi.
Mkuu wa
Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud (wa tatu kushoto), akiteta jambo na Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam na Zanzibar, Donatus Richard, wakati wa uzinduzi wa Tamasha la Vyakula na Rasirimali za
Baharini (Zanzibar Sea Food Festival
2021) litakalofanyika Oktoba 8-9.
NA MWANDISHI WETU
BENKI
ya NMB imetangazwa kuwa Mdhamini Mkuu wa Tamasha la Rasirimali na
Vyakula vya Baharini Visiwa vya Zanzibar (Zanzibar Sea Food Festival
2021), linaloratibiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ),
kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Uzinduzi
wa Tamasha hilo umefanyika visiwazi Zanzibar leo, ambapo linatarajia
kuunguruma kwa siku mbili mfululizo hapo Oktoba 8 na 9 mwaka huu, katika
Fukwe za Kendwa, likiwakutanisha pamoja wasanii wa kitaifa na kimataifa
na wahudhuriaji zaidi ya 30,000, chini ya kaulimbiu: 'Kamata Mshipi,
Vumba ni Fursa.'
Akizungumza
wakati wa uzinduzi huo, Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam na
Zanzibar, Donatus Richard, alisema Beni yake inathamini jitihada za SMZ
za kuimarisha Uchumi wa Bluu na kwamba dhamira ya dhati ya kuunga mkono
jitihada hizo zimewachochea kukubali kudhamini tamasha hilo linaloenda
kuongeza thamani ya utalii visiwani humo.
"Tunashukuru
sana kwa fursa hii adhimu ya kuwa wadhamini wakuu wa tamasha hili la
Rasirimali na Vyakula vya Baharini, hii ni kwa sababu NMB inathamini
sana Sekta ya Utalii nchini. Na kwa kuthibitisha hilo, tumejikita zaidi
kusaidia harakati za za kufikia Uchumi wa Bluu, ambazo ziko chini ya
Serikali ya Zanzibar.
"Kwa
kuelewa umuhimu huo, wenyeji wetu ambao ni Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Kaskazini Unguja, ilipotuomba kudhamini, hatukusita kukubali, tukitambua
kuwa utalii unachangia uchumi, pamoja na asilimia 80 ya pesa za kigeni
katika hazina ya Serikali," alisisitiza Donatus.
Aliongeza
kuwa, wanaamini Zanzibar Sea Food Festival lina umuhimu mkubwa katika
kukuza utalii na kuchangia pato la taifa na wao kama wadau wa maendeleo,
wanajisikia fahari kuwa sehemu ya mafanikio ya ukuzaji uchumi na kwamba
wamejipanga vya kutosha kutumia kila fursa ya kusaidia mchakato huo.
Akilitambulisha
tamasha hilo, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud,
alisema Zanzibar Sea Food Festival limebuniwa kwa lengo la kusapoti
juhudi za utekelezaji wa Sera za Serikali ya Zanzibar chini ya uongozi
wa Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Aliyataja
makundi yatakayoshiriki tamasha hilo kuwa ni pamoja na wavuvi, watalii,
wasanii, wawekezaji, watembeza wageni, taasisi za fedha, mashirika ya
Teknolojia ya Habari, Mawasiliano, Kampuni za vinywaji, hoteli za
kitalii, mikahawa na wananchi wa kada zote visiwani humo na Tanzania kwa
ujumla.
"Faida
mbalimbali zinatarajiwa kupitia tamasha hili, ambazo zitasaidia jamii ya
wana Kaskazini Unguja, kama vile mauzo ya samaki na mazao ya bahari
takribani tani 30, sanjari na kuwakutanisha na kuwaunganisha kibiashara
wavuvi wasiopungua 10,000 na wawekezaji wa hoteli za kitalii wasiopungua
127.
"Pia faida nyingine
zitokanazo na tamasha hilo ni ujenzi na ukarabati wa vyumba vya
madarasa visivyopungua 150, ajira za muda 16,322, ujenzi wa barabara ya
lami kilomita 2.5, maonesho ya kazi za wavuvi na wajasiriamali, pamoja
na kazi mbalimbali za uhifadhi wa mazingira," alibainisha Mahmoud.
Aliongeza
kuwa, tamasha hilo ambalo waratibu wenza ni pamoja na Clouds Media,
Kampuni za STR8UP Vibes na Zan Ocean, litapambwa na burudani kutoka kwa
wasanii wa kitaifa na kimataifa takribani 30, wakiwemo FireBoy wa
Nigeria, Focalist na DJ Obza wa Afrika Kusini, na wakali mbalimbali
kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
No comments:
Post a Comment