Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma.
Serikali ya Tanzania imetenga jumla ya shilingi bilioni 57.98 kwa ajili ya kuimarisha na kupanua fursa za upatikanaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.
Akitoa taarifa kwa umma leo, tarehe 23 Oktoba 2021, ofisini kwake jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako ameainisha kuwa utekelezaji wa Mpango huo katika Wizara yake utahusisha pia kuimarisha ujifunzaji na ufundishaji kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, ambapo Shilingi bilioni 1.54 zimetengwa, na kuimarisha mazingira ya utoaji wa Elimu ya Ualimu, ambapo kiasi cha Shilingi bilioni 5.41 zimetengwa, hivyo kufanya jumla ya Shilingi bilioni 64.93 za Mpango huo, ambazo matumizi yatasimamiwa na Wizara yake.
Akifafanua juu ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi, Prof. Ndalichako amesema kuwa zitatumika kukamilisha ujenzi na kununua na kusimika samani katika vyuo 25 vya Ufundi Stadi vya Wilaya, ambapo kiasi cha Shilingi bilioni 28.76 kimetengwa.
“Ukamilishaji wa Vyuo hivi vya Wilaya utawezesha ongezeko la takribani wanafunzi 30,000 katika Vyuo vya VETA”, amesema.
Ameyataja matumizi mengine kuwa ni kukamilisha ujenzi na kuweka samani katika Vyuo vinne (4) vya VETA vya ngazi ya Mkoa katika mikoa ya Njombe, Rukwa, Simiyu na Geita, ambapo Shilingi bilioni 18.70 zimetengwa. Prof. Ndalichako amesema kuwa vyuo hivyo navyo vitaongeza fursa za wanafunzi 5,600 katika mafunzo ya ufundi stadi na kukamilisha lengo la kila Mkoa kuwa na Chuo cha Ufundi Stadi kinachomilikiwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).
Vilevile Prof. Ndalichako amesema Serikali imepanga kutumia Shilingi bilioni 1.04 kujenga mabweni katika Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTCC), lengo likiwa ni kuongeza fursa za mafunzo ya Ualimu wa ufundi stadi ili kuendana na ongezeko la vyuo vya ufundi stadi nchini.
Sambamba na uendelezaji wa vyuo vya ufundi stadi, Prof. Ndalichako amesema Serikali imepanga kutumia Shilingi bilioni 6.8 kuimarisha Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (Folk Development Colleges-FDCs) kwa kununua mitambo na zana za kufundishia na kujifunzia katika vyuo 34, ikiwa ni miongoni mwa hatua za kuenzi kwa vitendo maono Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere. Mwalimu Nyerere alianzisha vyuo hivyo kwa ajili ya kutoa fursa kwa wananchi kujifunza katika mazingira yao na kwa kuzingatia rasilimali na fursa zilizopo katika maeneo yao.
Aidha, amesema kuwa katika kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji kwa vitendo katika Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), Shilingi bilioni 2.66 zimetengwa kwa lengo la kukamilisha Jengo moja la Chuo ambalo litakuwa na kumbi 2 za mihadhara, vyumba 6 vya madarasa, maabara 7 na ofisi 26.
Prof. Ndalichako alitoa shukrani za pekee kwa Rais wa Jamhuri wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kutambua umuhimu wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi na kuyapa kipaumbele kikubwa katika Serikali yake, akisema kuwa daima amekuwa akitenga fedha kwa ajili ya kuimarisha mafunzo hayo na kusisitiza kuona vijana wakipata mafunzo kwa vitendo.
“Uimarishaji wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi utawezesha kuandaa rasilimali-watu kwa maendeleo ya uchumi wa viwanda na kuongeza tija katika uzalishaji mali. Aidha, itachangia katika kupunguza tatizo la ajira kwa vijana na hivyo kutekeleza agenda ya maendeleo na ustawi wa jamii kwa ufanisi,” amesema.
Prof. Ndalichako amewaelekeza watendaji wa Wizara yake na wakuu wa taasisi zinazohusika na utekelezaji wa miradi hiyo, kuzingatia mambo mbalimbali ikiwemo kuandaa mpango kazi wa utekelezaji na kushirikisha wadau katika utekelezaji mpango huo. Ameagiza utekelezaji wa mpango huo uwe umekamilika ifikapo Mei 2022.
Tarehe 10/10/2021, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, alizindua Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO 19. Mpango huo una thamani ya Dola za Marekani milioni 567 sawa na Shilingi Trilioni 1.3 zilizotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa – IMF kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali inayolenga kuleta maendeleo kwa ustawi wa Taifa na kuwezesha mapambano dhidi ya UVIKO – 19.
Lengo lake kuu ni kufufua uchumi kutokana na athari za ugonjwa huo. Katika Mpango huo, Sekta ya Elimu imetengewa Shilingi bilioni 368.9 sawa na asilimia 28.5, ambapo OR – TAMISEMI imepewa Shilingi bilioni 304 kwa ajili ya miradi ya elimu. Tayari Waziri OR – TAMISEMI amekwishatoa taarifa ya mpango wa utekelezaji miradi mbalimbali itakayogharimiwa kwa fedha hizo.
No comments:
Post a Comment