HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 18, 2021

TFNC: Siku ya chakula, viribatumbo bado tatizo

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Dk. Germana Leyna, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Na Irene Mark


LICHA ya kupungua kwa maradhi ya utapia mlo kwa watoto chini ya miaka mitano, watanzania wanakabiliwa na tatizo la uzito uliopitiliza hali inayowaweka kwenye hatari ya kupata maradhi yasiyoambukizwa.


Akizungumza na wanahabari ofisini kwake Dar es Salaam leo Oktoba 18.2021 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Dk. Germana Leyna  alisema tatizo hilo lipo zaidi ya wanawake kutoka ukanda wa kaskazini mwa nchi yetu.


Katika mazungumzo hayo Dk. Leyna alikuwa akielezea kilele cha siku ya Lishe hapa nchini ambayo kitaifa inaadhimishwa Oktoba 23 mwaka huu, mkoania Tabora.


“Siku hii ya Chakula hapa nyumbani ilianza mwaka jana, hii ni mara ya pili tunaadhimisha lengo ni kuhamasisha ulaji sahihi unaojumuisha makundi yote ya chakula kwenye sahani moja.


“Tulianza kuadhimisha tangu Oktoba 18 na kilele chake ni Oktoba 23 kwenye viwanja vya Nanenane Ipuli kwa kaulimbiu isemayo ‘Lishe bora ni Kinga Thabiti ya Magonjwa. Kula Mlo Kamili, Fanya Mazoezi, Kazi iendelee’ tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi ili kujifunza.


“Kula mlo kamili sio lazima uwe na uwezo kiuchumi, vyakula vingi vinapatikana kwenye maeneo yetu ni kiasi cha kujua tu kama huna nyama ni chakula gani kipo kwenye kundi hilo,” anasisitiza Dk. Leyna.


Anasema hali ya lishe inaimarika licha ya changamoto za mabadiliko ya mtindo wa maisha yanayosababisha watu wengi kuwa na uzito uliopitiliza ama kiribatumbo.


“Tatizo la uzito uliokithiri kwa wanawake walio katika umri wa kuzaa limeongezeka kutoka asilimia 29.7 kwa 2014 hadi 31.7 kwa takwimu za 2018, uzito uliozidi na kiribatumbo ni chazo kikuu cha magonjwa sugu yasiyoambukiza yanayosababishwa na ulaji duni na mtindo mbaya wa maisha magonjwa hayo kama kisukari, figo, moyo na baadhi ya saratani.


“Ni kweli kiribatumbo ni tatizo kwa wanawake hasa wa mikoa ya kaskazini hasa Kilimanjaro ambako hadi asilimia 49 ya wanawake wanaviribatumbo... na Dar es Salaam pia ipo kwenye mikoa kinara ya wanawake wenye viribatumbo,” anasema mkurugenzi huyo.


Awali alibainisha kwamba kiwango cha Udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano kimepungua kutoka asilimia 34.7 kwa mwaka 2014 hadi asilimia 31.8 kwa mwaka 2018.


Akinukuu takwimu za Shirika la Afya duniani (WHO 1995) licha ya kupungua kwa viwango vya utapiamlo lakini shirika hilo linaonesha kuwa hali ya lishe si nzuri, kwa kuwa wapo watoto zaidi ya milioni tatu waliodumaa hapa nchini.


Dk. Leyna alisema watoto wenye udumavu wapo zaidi kwenye mikoa 11 ambayo ni Dar es Salaam, Kagera, Kigoma, Mara, Dodoma, Geita, Tanga , Ruvuma, Mbeya, Morogoro na Tabora.


"Mikoa inayoongoza kwa utapiamlo ni mikoa inayozalisha mazao ya chakula na kufanyabiashara, sio kuweka mezani na kula, hivyo nishauri jamii kuzalisha mazao na kuweka mezani sio kufanyia biashara tu.”


Alisema siku ya lishe ni muhimu zaidi kwa wananchi ili kuongeza ufahamu wao kuhusu mlo kamili kama msingi wa afya bora na maendeleo ya kiuchumi na kijamii.


Kwa mujibu wa Dk. Leyna, maadhimisho ya mwaka huu yametanguliwa na shughuli mbalimbali za afya na lishe kuanzia Oktoba 18 hadi Oktoba 22,2021 huku bidhaa na vyakula vilivyoo gezwa virutubishi kutoka sambani au kiwandani zikiwa moja ya sehemu ya maonesho hayo.


Alisema kiwango cha ukondefu kimepungua kutoka alisimia 3.8 kwa mwaka 2014 hadi kufuikia asilimia 3.5 kwa mwaka 2018 na kupungua kiwango hicho lakini wapo watoto 600,000 wanautapiamlo mkali na wakadiri. 


“Huku tatizo la uzito pungufu likiwa limeongezeka kutoka asilimia 13.4 kwa mwaka 2014 hadi asilimia 14.6 kwa mwaka 2018... tatizo la upungufu wa damu miongoni mwa wanawake walio katika umri wa kuzaa ambao ni miaka 15 hadi 49 limepungua kutoka asilimia 44.8  hadi asilimia 28.8.”


Dk. Leyna alisema lishe bora huimarisha kinga ya mwili na hivyo husaidia kupunguza ukali wa maradhi na vifo vitokanavyo magonjwa ya kuambukiza.

No comments:

Post a Comment

Pages