Na Lydia Lugakila, Kyerwa
Baraza la Halmashauri ya wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera kupitia Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Rashid Mohamed Mwaimu limemkabidhi kiasi cha zaidi ya shilingi laki 5 kama msaada kwa mwanamke Alinda Wiliam aliyejifungua watoto 3 mapacha baada ya kutelekezwa na mume wake.
Kiasi hicho cha fedha kimepatikana kupitia harambee iliyoendeshwa na mkuu huyo wa wilaya katika kikao cha madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Rweru plaza.
Akikabidhi msaada huo mkuu wa wilaya hiyo Rashid Mwaimu amempongeza mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 21 mkazi wa Kitoma Kitwechenkura kwa kujifingua salama huku akimtaka kuweka juhudi katika kuwalea watoto hao na kuahidi kuwa naye bega kwa bega.
"Watoto ni wetu sote na ni watoto wa Mheshimiwa Rais Samia tuwalee sote sababu Watanzania wote ni ndugu" alisema Mwaimu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Bahati Henerco kupitia Baraza hilo amewapongeza madiwani hao pamoja na mkuu wa wilaya hiyo kwa kujitoa kwao kunusuru maisha ya mwanamke huyo anayedaiwa kutelekezwa na mume wake tangu alipojifungua watoto hao huku akimuhimiza kubadilisha fedha hiyo kuwa mali ili aanzishe biashara itakayo muingizia kipato na kuendelea kuwatunza watoto hao.
Bi Alinda William alijifungua watoto 3 mmoja wa kike wawili wa kiume katika hospitali ya Kitwechenkura iliyopo wilayani humo na kutekelezwa na mume wake aliyefahamika kwa jina la Tumaini Morice mwenye umri wa miaka 25 kutokana na maisha ya familia hiyo kuwa magumu.
Hata hivyo kwa upande wake diwani wa kata Rukuraijo Bi Gisera Bruno ameiomba halmashauri hiyo kuendelea kumfuatila zaidi mama huyo ili watoto hao wafikie hatua mzuri.
No comments:
Post a Comment