HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 28, 2021

Benki zaahidi kuongeza ukopeshaji kuukwamua uchumi


Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB - Ruth Zaipuna akiwasilisha mada juu ya wajibu wa serikali, taasisi za fedha na sekta binafsi katika kuongeza upatikanaji wa mikopo na mchango wa wadau katika kufufua ukuaji wa uchumi kwenye mkutano Mkuu wa 20 wa Taasisi za Fedha Nchini uliofanyika mwishoni mwa juma jijini Dodoma uliondaliwa na Benki Kuu (BOT).

 

 Na Mwandishi Wetu

 

Licha ya ukopeshaji nchini kuathirika na janga la Uviko-19, benki zimeahidi kuongeza mikopo kwa ajili ya sekta binafsi kufuatia kuimarika kwa uchumi wa dunia na hatua zinazochukuliwa na serikali kuweka sawa huduma hiyo.

 

Taasisi hizo za fedha ziliweka bayana mpango huo Ijumaa jijini Dodoma kwenye Mkutano wa 20 wa Taasisi za Fedha (COFI 2021) nakusema kuimarisha ukopeshaji kutasaidia uzalishaji na kuukwamua uchumi wa taifa kufuatia janga la Uviko-19.

 

Kwa mujibu wa viongozi waandamizi wa benki hizo, hilo litawezekana kwa sababu benki nchini zina uwezo kifedha kukopesha zaidi na tena kwa riba rafiki.

 

Ili yote hayo yaweze kufanyika kwa ufanisi, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi Ruth Zaipuna, alisema juhudi za pamoja ni muhimu na ushirikiano wa wadau wote unahitajika.

 

“Janga la Uviko-19 limekuwa na athari kubwa kwenye benki zetu kuikopesha sekta binafsi,” kiongozi huyu aliwaambia washiriki wa COFI 2021 wakati anawasilisha maada kuhusu kuongeza mikopo kwa sekta binafsi baada ya janga la Uviko-19.

 

Wasilisho lake lilikijita kwenye wajibu wa serikali, taasisi za fedha na sekta binafsi katika kuongeza upatikanaji wa mikopo na mchango wa wadau hao kufufua ukuaji wa uchumi.

 

“Ili kuchochea ukopeshwaji wa sekta binafsi baada ya janga la Uviko-19, mambo kadhaa yanabidi kufanywa na wadau husika. Hatua hizi zinahitaji mbinu shirikishi ili kuhakikisha matokeo endelevu ya kiuchumi,” Bi Zaipuna alisisitiza.

 

Aidha, alisema tayari kuna mazingira wezeshi ya kuongeza mikopo na ustahimilivu stahiki wa kisekta wa kuchochea kufufua ukopeshaji.

 

Hii ni pamoja na kuendelea kuimarika kwa uchumi wa dunia ambao baada ya kupigika na uviko hadi kudorora kwa asilimia 3.1 mwaka 2020 sasa Shirika la Fedha Dunia (IMF) linasema utakua kwa asilimia 5.9 mwaka huu.

 

Kuimarika huko kutapelekea uchumi wa Tanzania nao pia kufanya vizuri ukikua kwa asilimia tano mwaka huu ukilinganisha na ukuaji wa 2020 wa asilimia 4.8.

 

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof Florens Luoga alisema hali itakuwa nzuri zaidi 2022 kutokana na kupungua kwa athari za Uviko-19 kutakaopelekea uchumi wa taifa kukua kwa asilimi 5.2 mwaka kesho.

 

Mkutano wa 20 wa Taasisi za Fedha uliofunguliwa rasmi na Rais Samia Suluhu Hassan uliandaliwa na BoT kwa kushirikiania na Umoja wa Mabenki nchini (TBA) ili kujadili uimarishaji wa uchumi wa Tanzania kufuatia janga la Uviko-19.

 

Bi Zaipuna alisema sababu nyingine ya kuwepo mazingira sahihi ya kufufua ukopeshaji ni kutokana na sera sahihi za serikali ambazo pamoja na kutoa kinga madhubuti dhidi ya Uviko-19 pia zimesaidia sekta ya benki kustahimili vishindo vya janga hilo.

 

Ustahimilivu huo ulipelekea rasimali fedha za benki nchini kuongrezeka kwa asilimia 4.16 mwaka 2020 hadi TZS trilioni 34.68 huku amana nazo zikiongezeka karibu kwa asilimia nne hadi TZS trilioni 24.77.

 

Mitaji nayo ilendelea kuwa sawa mwaka jana na karibu benki zote zilipata faida zikiongozwa na NMB iliyopata faida kubwa kuwahi kutengenezwa na benki yoyote nchini ya TZS bilioni 206.

 

“Hali hii ilizifanya benki kuendelea kulihudumia taifa kipindi chote za janga la Uviko-19 bila kuathiri wateja na wafanyakazi wake,” Bi Zaipuna alisema na kuongeza kuwa taasisi hizo pia zilichangia juhudi za taifa za kukabiliana na Uviko kwa kuchangia zaidi ya TZS bilioni moja.

 

Benki zilihimiza matuzimizi mbadala ya kufanya malipo na kupanua wigo wa huduma za kifedha za kidigitali kwa kuongeza vikomo vya miamala na kufuta kabisa baadhi ya tozo.

 

Hatua hizo ziliongeza kwa kiasi kikubwa idadi na thamani ya miamala ya kieletroniki ambayo mwaka 2020 ilifikia TZS trilioni 126 kutoka TZS trilioni 99 mwaka uliotangulia.

 

“Ukuaji huu kwa kiasi fulani ulitokana na hatua za kisera za BoT za kuhimiza huduma za kifedha za kidijitali, zikiwemo kuongeza miamala ya pesa mtandao na vikomo vyake,” Bi Zaipuna alisema.

 

Hatua nyingine za kisera zilizochukuliwa na BoT mwaka 2020 ni pamoja na kupunguza riba za hati fungani za serikali na kupunguza hadi asilimia sita kiwango cha sehemu ya amana za benki kinachotakiwa kuwekwa benki kuu (SMR).

 

BoT pia ilishusha riba ya mikopo kwa benki (discount rate) hadi asilimia tano kuzipunguzia gharama za kukopa na kuziongezea ukwasi. Hatua nyingize za kisera zilichukuliwa Julai mwaka huu ili kuongeza msukomo wa kasi ya kuikopesha sekta banafsi na kuharakisha ufufuaji wa uchumi.

 

Hatua hatua hizo ni pamoja na kulegeza masharti ya usajili wa mawakala wa benki, ukomo wa riba kwenye akaunti za makampuni ya watoa huduma za

fedha kwa njia ya simu za mkononi na kuanzishwa kwa mfuko maalum wa kuzikopesha benki na taasisi za fedha wenye thamani ya TZS trilioni moja.

 

“Hatua hizi zilizochukuliwa na BoT Julai 2021 na kuimarika kwa uchumi wa dunia kumepelekea kuongezeka kwa kiasi kikubwa ukopeshaji wa sekta binafsi,” Bi Zaipuna alifafanua.

 

Kabla ya Uviko-19 mikopo kwa ajili ya sekta binafsi ilikuwa inakua vizuri na kifikia asilimia 11.1 mwishoni mwa mwaka 2019 lakini hali ilibalika ghafla baada ya dunia kugubukwa na janga hilo.

 

Ukuaji huo ulipungua hadi asilimia 5.5 katikakti ya mwaka jana na hali ilizidi kuwa mbaya miezi iliyofuata. Bi Zaipuna alisema kumekuwepo na maendeleo mazuri hivi karibuni kutokana na kendelea kuimarika kwa uchumi wa dunia na jitihada za serikali pamoja na benki kuimarisha na kurahisisha upatikanji wa mikopo.


No comments:

Post a Comment

Pages