Mkuu wa Idara ya Biashara za Kadi wa Benki ya NMB, Philbert Casmir
na Mratibu wa Bidhaa Selcom, Gallus Runyeta wakibadilishana nyaraka
baada ya kutiliana saini ya makubaliano ya ushirikiano wa kimalipo kati
ya Benki ya Nmb na Selcom, mkoani Dar es Salaam. Kulia ni Mkuu wa Idara ya Wateja Maalum, Getrude Mallya na kushoto ni Mwandamizi kitengo cha Biashara za Kadi, David Ngusa.
Mkuu wa Idara ya Biashara na Kadi wa Benki ya NMB, Philbert Casmir na Mratibu wa Bidhaa Selcom, Gallus Runyeta wakionyesha mikataba baada ya kutiliana saini ya makubaliano ya ushirikiano wa kimalipo kati ya Benki ya Nmb na Selcom, jmkoani Dar es Salaam. Kulia ni Mkuu wa Idara ya Wateja Maalum, Getrude Mallya na kushotoMwandamizi kitengo cha Biashara za Kadi, David Ngusa.
Na Mwandishi Wetu
Kuifanya Tanzania kuwa taifa la uchumi wa kidijitali lenye matumizi madogo ya pesa taslimu kunahitaji ushirikiano wa karibu wa wadau, ubunifu wa hali ya juu na uwekezaji stahiki katika teknolojia mpya za kisasa.
Uhalisia huo umetabainishwa jana jijini Dar es Salaam na maafisa waandamizi wa Benki ya NMB na kampuni ya Selcom Tanzania walipokuwa wanatangaza kushirikiana kwa taasisi zao kusaidia kupunguza matumizi ya pesa taslimu nchini.
Akiutaja ushirikiano huo kuwa maendeleo makubwa, Mkuu wa Idara ya Biashara za Kadi wa NMB, Bw Philbert Casmir, alisema benki hiyo imekuwa mstari wa mbele kwenye mapinduzi ya malipo nchini.
Pia kiongozi huyo alisema ubia huo unawapa wateja wa NMB na Selcom pamoja na wamiliki wa simu za mkononi mawanda mapana zaidi ya sehemu za kufanyia malipo na kuchagua namna ya kulipia bidhaa na huduma mbalimbali.
Kutokana na hatua hiyo, sasa wateja wa NMB wanaweza kuvitumia vituo vya miamala vya Selcom kufanya manunuzi na wamiliki wa simu za mkononi kufanya malipo kupitia mfumo wa msimbo wa NMB (QR Codes) ambao pia utatumiwa na wateja wa Selcom.
Wakati NMB ina zaidi ya sehemu 53,000 kwenye mtandao wake wa mfumo wa malipo wa msimbo, Selcom ina karibu idadi kama hiyo ya vituo vya kufanyia miamala nchini kote.
“Ubia wa kimkakati na ubunifu kama huu ni muhimu katika kufikia ndoto ya kuifanya Tanzania kuwa jamii ambayo imeachana na matumizi ya fedha taslimu, na tutaendelea kujitolea kwa hali na mali kubuni suluhisho za malipo zinazoendana na hali halisi na mahitaji ya soko,” Bw Casmir alisema.
Aidha, aliongeza kuwa lengo mama la ushirikiano huo ni kuimarisha huduma jumuishi za kifedha nchini, kujenga mfumo mpana wa malipo, na kuongeza wigo wa suluhisho za malipo za kisasa.
Kufanikiwa kwa azma hii vile vile kunahitaji uwepo wa mazingira mazuri ya mfumo jumuishi wa kufanya malipo haraka, kitu ambacho Bw Casmir alisema pia ni lengo mojawapo la ubia wa NMB na Selcom.
“Tunafurahi kushirikiana na Selcom ili kuimarisha zaidi mfumo jumuishi wa haraka wa kufanya malipo nchini Tanzania. Kupitia ushirikiano huu, tunawatengenezea wateja wetu na wa kampuni za simu fursa kubwa ya kufanya malipo kisasa zaidi,” alisisitiza.
Hadi Juni 30, 2021, wamiliki wa simu za mkononi nchini walikuwa milioni 53.1 ambao kati yao takriban milioni 33.3 walikuwa wameuganishwa na huduma ya pesa mtandao.
Kwa mujibu wa Mratibu wa Bidhaa wa Selcom, Bw Gallus Runyeta, mfumo wa msimbo (QR Code) unasaidia sana kurahisisha miamala katika biashara na teknolojia yake imekuwa nyeti kwenye kufanya malipo na kujenga uchumi wa kidijitali.
Alisema QR Code inasaidia sana kuondoa haja ya mtu kutembea na fedha taslimu kwani huduma nyingi muhimu tayari zimeunganishwa na mfumo wake, mathalani maduka makubwa, sheli na hata migahawa.
Aidha, Bw Runyeta alitabainisha kuwa ubia wa Selcom na NMB kwenye hili unasaidia kupanua zaidi mfumo jumuishi wa haraka wa kufanya malipo kidijitali na kuongeza fursa zinazopatikana ndani yake kutokana na wigo mpana wa sehemu na vituo vyao vya malipo.
No comments:
Post a Comment