........................................
MAJUMUISHO 12 na Mapendekezo nane yakifanyiwa kazi tofauti za kijinsia katika shughuli za uhifadhi wa misitu ya asili uvunaji na utumiaji wa rasilimali zinazopatikana katika misitu ya asili yataleta tija.
Hayo yalisemwa na Mtafiti na Mtaalamu wa Masuala ya Jinsia kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Profesa John Jeckoniah wakati akizungumza na waandishi wa habari ambao wapo katika ziara ya kujifunza kuhusu utekelezaji wa usimamizi Shirikishi wa Misitu Mkoa wa Morogoro na Lindi.
Alisema mapendekezo hayo yalijiri baada ya kufanya utafiti ili kujua mgawanyo wa majukumu katika shughuli za uhifadhi wa misitu ya asili na ushiriki wa makundi mbalimbali ya kijinsia kufikia rasilimali zitokanazo na misitu ya asili.
"Lengo lingine la utafiti huo tulioufanya katika Wilaya ya Kilosa, Mvomero na Morogoro Vijijini ulilenga kuibua masuala gani ya muhimu ya kijinsia ambayo yapo kwenye shughuli nzima za uhifadhi wa misitu ya asili inayosimamiwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu (MJUMITA) kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uswis (SDC) " alisema Jockeniah.
Alitaja lengo lingine kuwa ni kutaka kuangalia kuna uelewa gani kuhusu kutumia rasilimali mbalimbali zilizopo kwenye misitu ya asili.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika ziara hiyo baadhi ya wajumbe wa kamati za maliasili wa Kijiji cha Ndole kilichopo Kata ya Kinda wilayani Mvomero mkoani hapa na Wajumbe wa Kijiji cha Ihombwe wilayani Kilosa walilishukuru shirika la TFCG kwa kuwapatia mafunzo ya uhifadhi wa Misitu.
Kaimu Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Ndole Ezekiel Isaya alisemia baada ya kupata elimu hiyo Jamii imekuwa na uelewa mpana wa uhifadhi misitu na matumizi bora ya ardhi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Jamii wa kijiji hicho Mathias Chambo alisema licha ya kupanga matumizi bora ya ardhi na mpango wa mkaa endelevu changamoto kubwa ni soko la kuuza bidhaa hiyo baada ya wafanyabiashara kuacha kwenda kuinunua.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maliasili wa kijiji hicho Anna Mohamed alisema baada ya kupata elimu hiyo hivi sasa wanawake wamekuwa wakishiriki katika biashara ya mazao ya misitu kama wanavyofanya wanaume hivyo kutekeleza dhana nzima ya kuzingatia jinsia.
No comments:
Post a Comment