Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge (katikati), akijadiliana jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy (kulia) wakati viongozi hao walipokuwa katika ziara ya kazi mkoani Ruvuma jana.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akisisitiza jambo wakati alipokuwa akizungumza na Ujumbe wa Viongozi Wakuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (hawapo pichani), walipomtembelea ofisini kwake wakiwa katika ziara ya kazi mkoani humo jana. Ujumbe huo uliongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wakili Julius Kalolo.
Na Veronica Simba - REA
Uongozi wa Juu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), umetoa ahadi kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge kuwa miradi ya nishati vijijini inayotekelezwa katika mkoa huo itasimamiwa kikamilifu na kuleta matokeo chanya kwa wananchi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika kikao na Mkuu wa Mkoa ofisini kwake, Novemba 22 mwaka huu, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Wakili Julius Kalolo na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy walisema kuwa Wakala umejipanga kushughulikia changamoto zote zilizojitokeza katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Awali, Mkuu wa Mkoa aliwaeleza viongozi hao uwepo wa changamoto ya Mkandarasi Namis Corporate Ltd kutotekeleza kwa kasi inayotakiwa, Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza.
Akieleza mkakati uliowekwa kutatua changamoto hiyo, Wakili Kalolo alieleza kuwa, Bodi imemtaka Mkandarasi husika kuhakikisha anakamilisha Mradi huo, siyo zaidi ya Desemba 31, 2021 vinginevyo atachukuliwa hatua za kimkataba.
Vilevile, Mkandarasi huyo ameagizwa kutengeneza Mpango-Kazi wa kila wiki ukionesha kazi atakayoifanya, atawasha umeme katika kijiji gani na muda gani na kuuwasilisha kwa Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ambako kazi inafanyika pamoja na Diwani wa eneo husika ili waweze pia kufuatilia utekelezaji wake.
Aidha, alisema kuwa Bodi imemwagiza Mkandarasi kuongeza magenge ya kazi na kuhakikisha hayapungui matano pamoja na kuongeza wafanyakazi wenye ujuzi na kujituma ili kazi iweze kukamilishwa kwa wakati.
Akieleza zaidi, Mwenyekiti wa Bodi alisema imebainika kuwa Mshauri Mwelekezi wa Mradi amechangia pia katika ucheleweshwaji wa Mradi kutokana na kutotekeleza wajibu wake ipasavyo, hivyo Bodi imemwagiza kubadilika mara moja na kutimiza wajibu wake kikamilifu.
“Yeye ndiye anapaswa kututaarifu sisi kuhusu utendaji kazi wa Mkandarasi lakini hakuna ripoti yoyote aliyoileta rasmi kueleza matatizo ya Mkandarasi.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa REA alitumia fursa hiyo kutoa maelekezo kwa Wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini nchini kote kuwa Serikali haitatoa muda wa nyongeza wa kukamilisha miradi hiyo.
Pia, aliwasisitiza kuhakikisha wanafanya kazi kwa kadri ya michoro ilivyo na endapo kutakuwa na tofauti yoyote basi ni lazima kwanza wapitie TANESCO na kwa Mshauri Mwelekezi kabla hawajabadilisha mchoro wowote.
Vilevile, aliwataka kuhakikisha wanawadhibiti wafanyakazi wao kutojihusisha na vitendo vyovyote vya rushwa na matumizi ya lugha zisizofaa pamoja na kuwazuia wafanyakazi hao kujihusisha.
na kazi za kufanya ‘wiring’ katika nyumba za wananchi na majengo mbalimbali kwani ni kinyume cha mkataba.
“Hii ni miradi ya serikali hivyo ni lazima itekelezwe kwa kuzingatia taratibu,” alisisitiza Mhandisi Saidy.
Aidha, aliwataka wakandarasi kuhakikisha wanaagiza na kutumia vifaa vyenye ubora huku akisisitiza kuwa mkandarasi atakayetumia vifaa visivyo na ubora ajue kuwa anafanya hivyo kwa gharama zake binafsi.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza na wa Pili mkoa wa Ruvuma, Msimamizi wa Miradi ya REA Kanda ya Kusini, Mhandisi Daniel Mwandupe alieleza kuwa, mzunguko wa kwanza wa mradi hadi kukamilika kwake, utagharimu shilingi za kitanzania 43,869,003,071.89 na fedha za kimarekani dola 7,483,076.98.
Alisema kuwa, katika mzunguko wa kwanza wa mradi, vijiji 144 vimepatiwa umeme kati ya vijiji 177 sawa na asilimia 81.4. Aidha, wateja 7,004 wa awali wameunganishwa kati ya lengo la kuunganisha wateja 9,778 mradi utakapokamilika.
Kwa upande wa mzunguko wa pili wa mradi, Mhandisi Mwandupe alieleza kuwa jumla ya vijiji 265 vya mkoa wa Ruvuma ambavyo havijafikiwa na umeme kati ya 554 vilivyopo, vitapelekewa umeme na kuunganisha wateja wa awali 5,170. Mradi utagharimu shilingi za kitanzania bilioni 71.95.
Katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa aliushukuru Uongozi wa REA na wa Wizara ya Nishati kwa ujumla wake, kwa ushirikiano mzuri ambao wamekuwa wakiutoa kwa Ofisi yake katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini na Mkurugenzi Mkuu wa REA, wako katika ziara kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati vijijini katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara, Lindi na Pwani.
No comments:
Post a Comment