Na Dotto Mwaibale, Singida
VIJANA Mkoa wa Singida wametakiwa kujikita kwenye kilimo chenye tija cha zao la alizeti ili kufanikisha mkakati wa kuongeza uzalishaji wa zao hilo na kuondoa changamoto ya uagizaji wa mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.
Upungufu wa mafuta ya kupikia unaligharimu Taifa zaidi ya Sh.Bilioni 474 kwa mwaka ambapo tani zinazokadiriwa kufikia 365,000 hutumika kuagiza mafuta ya hayo nje ya nchi.
Hayo yamebainishwa na Afisa Vijana Mkoa wa Singida Frederick Ndahani wakati akizungumza na vijana wa Kata ya Mtinko na Kijota za Halmshauri ya Wilaya ya Singida alipotembelea jana wakati wa mafunzo ya biashara kwa vijana hao.
" Vijana mnatakiwa kuto chezea fursa ya kilimo cha zao la alizeti kwani kitawainua kiuchumi" alisema Ndahani.
Akiwa Katika mafunzo hayo Ndahani alisema Serikali imetoa ruzuku ya mbegu ya alizeti kupitia Wakala wa Uzalisha wa Mbegu (ASA) ambayo itaweza kupatikana kwa sh.3500 kwa kilo moja badala ya sh. 35000 iliyokuwa ikitumika msimu wa kilimo uliopita.
Ndahani aliwaondoa hofu vijana hao kwa kuwaeleza kuwa soko la bidhaa hiyo kuwa lipo kwani Mkoa wa Singida una viwanda vya alizeti vipatavyo 240 vya kuchakata mbegu hizo na moja ya kiwanda hicho ni cha Mount Meru ambacho ni kikubwa Afrika Mashariki na kiwa kinahitaji Tani 1000 za alizeti kwa siku ambazo hazipatikani.
Alisema Mkoa wa Singida umekuwa na miundombinu mizuri ya barabara zinazounganisha mikoa yote nchini hivyo biashara ya mafuta pamoja na mashundu ya alizeti hayawezi kukosa soko ndani na nje ya mkoa.
No comments:
Post a Comment