HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 22, 2021

SKAUTI RUKWA KUPAMBANA NA RUSHWA



 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (katikati) akiwa ameshika nakala ya Mwongozo wa Mafunzo kwa Vijana wa Skauti kuhusu mapambano dhidi ya Rushwa leo ofisini kwake Sumbawanga. Wa kwanza kulia ni Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Rukwa Daniel Ntera akifuatiwa na Kamishna wa Skauti Rukwa Hamis Kikoloma na wa kwanza kushoto ni Afia Elimu Mkoa wa Rukwa Samson Hango. 

 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joseph Mkirikiti amewataka Maafisa Elimu Wilaya  kutumia mwongozo wa mafunzo kwa vijana  wa skauti kufundisha uzalendo na uadilifu hatua itakayowasaidia kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa kuanzia shule za msingi hadi vyuo.

Ametoa kauli hiyo leo (20.11.2021) wakati akiwakabidhi Wakuu wa Wilaya za Nkasi, Kalambo na Sumbawanga Mwongozo wa mafunzo kwa Vijana wa skauti kuhusu kuzuia  na Kupambana na rushwa utakaotumika kwenye shule za msingi ,sekondari na vyuo kote mkoani Rukwa kwenye hafla iliyofanyika mjini Sumbawanga.

Mkirikiti aliongeza kusema Wakuu wa Wilaya wana wajibu wa kwenda kuhakikisha mwongozo huo unatumika na kufikia Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata ili vijana wengi wapate elimu hiyo kupitia walimu wao.

“Elimu ya kudhibiti rushwa kwa watoto wa shule ni jambo muhimu kwani wakijengwa katika msingi wa kuishi bila rushwa watakuja kuwa raia wema na pia viongozi wazalendo na waadilifu kwenye jamii” alisisitiza Mkirikiti.

Katika hatua nyingine Mkirikiti ameonya kuongezeka kwa vitendo vya wanafunzi wa kike kupatiwa mimba hatua inayodumaza jitihada za kuendelea na masomo na kuwa vitendo hivyo ni kuwanyima haki ya elimu wanafunzi hao.

Alitaja wilaya ya Nkasi kuwa inaongoza kwa matukio ya wanafunzi wa kike kuripotiwa kutoendelea na shule kwa kupata mimba ambapo katika mwaka 2021 jumla ya wanafunzi 25 walipata mimba huku wilaya za Kalambo na Sumbawanga zikiwa zimeripoti matukio nane (8) kila moja.

“Nataka Afisa Elimu Mkoa na timu yako kwenye wilaya nendeni mkatumie uwepo wa skauti kudhibiti vitendo vya mimba za utotoni na kuwa hatutaki kuona walimu wanaoshabikia mimba kwa watoto wa shule” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.

Kwa upande wake Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Rukwa Daniel Ntera alisema lengo la kuwashirikisha skauti kwenye mapambano dhidi ya rushwa ni kuwafanya vijana watimize wajibu wao kwa msingi wa uwajibikaji, uwazi na uzalendo kwa taifa.

Ntera aliongeza kusema mwongozo huo ulioandaliwa na Takukuru kwa ushirikiano na Wizara ya Elimu utasaidia kufundisha dhana ya rushwa na hongo, juhudi za serikali katika kudhibiti rushwa na mapambano dhidi ya rushwa ya ngono.

“Mwongozo huu wa mafunzo utasaidia vijana wa skauti kupata elimu ya kutosha itakayowasaidia kuunga mkono juhudi za serikali ya Awamu ya Sita katika mapambano dhidi ya rushwa nchini” alisema Ntera.

Naye Kamishna wa Skauti Mkoa wa Rukwa Hassan Kikoloma akizungumza kwenye hafla hiyo alitaja malengo ya uwepo wa skauti kuwa ni kuandaa vijana kuwa raia wema wakue wakiwa na maadili na uzalendo kwa taifa.

Kikoloma alitoa ombi kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri za Rukwa kutoa ushirikiano na misaada ya kuwezesha shughuli za vijana hao ili kuleta tija na malengo ya kupambana na rushwa kwenye jamii yafikiwe na hatimaye maendeleo ya wananchi.

Halfa hiyo ya uzinduzi wa mwongozo wa mafunzo kwa vijana wa skauti ngazi ya Mkoa wa Rukwa kuhusu kuzuia na kupambana na rushwa yamehudhuriwa na Katibu Tawala Mkoa Denis Bandisa na  Wakuu wa Wilaya za Nkasi  Peter Lijuakali, Tano Mwera (Kalambo) na Sebastian Waryuba (Sumbawanga) , Makamanda wa Takukuru Wilaya, Maafisa Elimu na Waratibu Elimu Kata pamoja na vijana wa skauti .


No comments:

Post a Comment

Pages