HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 07, 2021

Rais Samia mgeni rasmi Mkutano wa Demokrasia ya Vyama vya Siasa na Maadhimisho Miaka 60 ya Uhuru

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatib akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam kuhusu Mkutano wa Vyama vingi vya Siasa na Maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru utakaofanyika Dodoma.
 
 
Na Hussein  Ndubikile, Dar es Salaam

Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kuwa mgeni rasmi na kufungua Mkutano wa Wadau wa Demokrasia ya Vyama Vingi vya Siasa na Maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru utakaofanyika Disemba 16 hadi 17 mwaka huu mjini Dodoma.

Akizungumza na wanahabari  jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatib amesema awali mkutano huo ulitakiwa kufanyika Oktoba 21 hadi 23 na kwamba kutokana na sababu za msingi uliahirishwa na kwamba upo hivyo wadau wamekumbushwa kwenda kushiriki kikamilifu.

Amebainisha kuwa mkutano huo utatanguliwa na Semina ya siku moja kwa wajumbe wa baraza hilo itakayofanyika Disemba 15 katika jiji hilo itakayolenga historia na majukumu ya baraza.

Amesisitiza kuwa mkutano huo ni muhimu kwani utawawezesha wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa kukutana na kubadilishana mawazo na uzoefu ili kuwezesha sheria zinazoratibu shughuli za vyama vya siasa nchini kuboreshwa kama itahitajika.

Ameongeza kuwa wadau watajadili utekelezaji wa sheria hizo sambamba na kudumisha amani, utulivu, uzalendo na umoja wa taifa na kwamba kutokana umuhimu wa mkuatano wamemualika Rais Samia kuwa mgeni rasmi na kuufungua.

Amefafanua kuwa mkutano utajumuisha wadau mbalimbali vya vyama hivyo ikiwamo wajumbe wa baraza la vyama vya siasa, Viongozi wa Kitaifa wa Vyama vya Siasa ambao siyo wajumbe wa baraza hilo, Viongozi wa dini Ngazi ya Taifa, Taasisi zisizo za Serikali, Viongozi wa Serikali, Waandishi wa Habari na Taasisi za Serikali na Watu Mashuhuri.

Mwenyekiti huyo amesema kuwa mada tatu zitawasilishwa na wataalamu wabobezi na kujadiliwa na wshiriki wa mkutano ikiwamo ya masuala ya kisheria, demokrasia, siasa,uchumi na maadili ya kitaifa, yanayohusiana na demokrasia ya vyama vingi vya siasa.

Amevishauri na kuvishauri vyama vyote vya siasa vyenye usajili kamili kuhudhuria mkutano huo, kwani washiriki watapata fursa adhimu kubadilishana mawazo kuhusu mambo yanavyovihusu na kwamba sasa ni ushawishi na hupatikana kwa njia ya majadiliano.

Aidha, amesema kwa kuwa mkuatno unafanyika wakati taifa linasherehekea miaka 60 ya uhuru, baraza hilo limeona ni vyema sualahilo likajadiliwa na kumpongeza Rais Samia na watanzania kwa ujumla kwa kutimiza miaka hiyo na hatua kubwa ya kimaendeleo waliyofikia.

Katika hatua nyingine, amempongeza Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Samia pamoja na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa jinsi wanavyoongoza nchi na kutupatia mafanikio zaidi ya kiuchumi, kijamii na kisiasa

Kwa upande wake, Mjumbe wa Baraza hilo, John Cheyo ametoa wto kwa watanzania kuendelea kudumisha uhuru na umoja wa nchi kwani mambo hayo ndio msingi imara amani na upendo.

Nae, Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili na Mahusiano wa Baraza la Vyama vya Siasa, Doyo Hassan Doyo amesema vyama vya siasa vinatakiwa kutambua kuwa baraza hilo lipo kwa mujibu wa sheria na lina uwezo wa kutatua changamoto zinazovikabili vyama vya siasa pamoja viongozi wa siasa.

Amewaasa viongozi wa siasa kuacha kutumia lugha za matusi zinazowakera watu na zinazohatarisha usalama wa nchi badala yake walitumie baraza kutatua changamoto zao.



No comments:

Post a Comment

Pages