Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe akizungumza wakati akifungua Kikao cha Mafunzo juu ya Matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa Ushuru wa Maegesho iliyotolewa na TARURA kwa Madiwani, Watendaji na Kamati hiyo.
Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam
Mkuu
wa Wilaya ya Kinondoni Godwin Gondwe amewaomba Wakala wa Barabara
Vijijini na Mijini (TARURA) alama elekezi zinazoonesha maeneo yao yote
ya maegesho ya magari ili kuondoa mkanganyiko kwa wananchi kuhusu Mfumo
wa Kielektroniki wa Ushuru wa Maegesho (TeRMIS) uliorejeshwa tena
kutumika kuanzia Disemba Mosi mwaka huu.
Hayo
ameyasema jijini Dar es Salaam wakati akifungua Kikao cha Mafunzo ya
matumizi ya mfumo huo iliyotolewa na TARURA kwa Madiwani, Watendaji wa
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni pamoja na Kamati ya Ulinzi na
Usalama ya Kinondoni.
Amesema wakati mfumo huo
umerejeshwa tena kuanza kutumika ni vyema wakala hao wakafikiria kuweka
alama kwenye maeneo ambayo mtu akipaki gari atatozwa ushuru huo ili
kuepuka msuguano kati yao na wateja.
"
Tunapoelekea mbeleni TARURA muweke alama za kuonyesha maeneo yenu
yanayohusika kutoza ushuru huu mkifanya hivyo mtaondoa malalamiko kwa
wateja," amesema DC Gondwe.
Amewapongeza TARURA
kwa kutoa elimu elimu ya mfumo huo jinsi unavyofanya kazi kwani
madiwani, watendaji na kamati hiyo watafikisha elimu kwa jamii.
Kwa
upande wake, Mtaalamu wa Mifumo ya Tehama wa TARURA, Shadrack Mahenge
amesema mfumo wa TeRMIS umeanzishwa na kurudishwa tena ili kudhibiti
upotevu wa mapato, wakandarasi wa ukusanyaji ushuru kuchelewa
kuwasilisha makusanyo kwa wakati pamoja na ugumu wa kupata taarifa
sahihi za mapato yaliyokusanywa.
Mahenge
amesema mfumo huo una faida nyingi ikiwemo ikiwemo kudhibiti ukwepaji
ushuru baada ya kuwekewa ankara, kuongeza mapato kwa Serikali na
upatikanaji wa taarifa za mapato yanayokusanywa.
Amefafanua
kuwa kwenye mfumo huo kuna maeneo yameboreshwa yakiwemo ya utoaji elimu
kupitia mitandao ya kijamii, Runinga, vipeperushi, matangazo ya
barabarani na mafunzo kwa makundi maalum.
Maboresho
mengine ni ulipaji wa ushuru ndani ya siku 14, faini ya Sh 10,000
kutoka Sh 30,000 baada ya siku hizo, ushuru kwa saa Sh 500 huku kwa
siku Sh 2500 kutoka Sh 4500 pamoja na kumbukumbu namba kupatikana ndani
ya saa moja.
Nae, Mwakilishi wa Meneja Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Lutufyo Mwakigonja amesema maoni,
mapendekezo yaliyotolewa wakati wa mafunzo hayo yatafikishwa sehemu
husika ili yafanyiwe kazi.
Mhandisi Lutufyo
amesema mafunzo hayo ni endelevu kwa kuwa ni muhimu katika kuhakikisha
elimu sahihi ya matumizi ya mfumo yanaeleweka kwa watumiaji.
Mstahiki
Meya wa Manispaa hiyo, Songoro Mnyonge amewapongeza TARURA na kwamba
elimu waliyopewa wataifikisha katika jamii ili kusaidia wananchi kupata
uelewa wa mfumo huo.
No comments:
Post a Comment