Mheshimiwa Majaliwa amesema wakati Serikali inaendelea na jitihada hizo ni vyema pia wananchi wakatumia mbolea mbadala zinazopatikana nchini kama ya Minjingu ili kukabiliana na uhaba uliopo.
“Serikali inaendelea na jitihada mbalimbali, na hivi karibuni tuliitisha kikao na waagizaji wote wa mbolea nchini na tumewaomba kuingiza mbolea kutoka katika maeneo mbalimbali duniani, ingawa Serikali inaendelea kufanya mawasiliano na nchi rafiki ili zisaidie katika kukabiliana na uhaba uliojitokeza ambao umetokana na kusimama kwa uzalishaji wa mbolea kutokana na janga la Uviko 19 duniani.”
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti leo (Jumanne, Novemba 30, 2021) akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Mbeya ambapo alipozungumza na wananchi eneo la la Kiwanja cha ndege cha zamani na alipokagua Ujenzi wa Shule ya Sekondari Mwashiwawala.
Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa mkoa huo kuendelea kuweka mipango ya kuboresha eneo la Uwanja wa ndege wa zamani wa Mbeya ambalo Mkoa umelitenga kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo wadogo wa jiji hilo kwa kutengeneza barabara na vizimba ili wafanyabiashara hao wafanye shughuli zao katika mazingira rafiki.
“Ndugu zangu wafanya biashara, nataka niwaambie nia ya dhati ya Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ya kutaka kuboresha biashara nchini kwa makundi yote ya wafanyabiashara wadogo, wa kati na wawekezaji wakubwa na ametuagiza wasaidizi wake tuendelee kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara wote ili wapate tija kutoka katika biashara zao.”
Awali akiwasilisha taarifa ya wafanyabiasha wadogo (Machinga) Makamu Mwenyekiti wa Machinga Taifa Bw. Ernest Massanja ameipongeza Serikali kwa namna ilivyoratibu zoezi la kuwapanga wafanyabiashara wadogo katika maeneo mbalimbali nchini “Tunamshuruku sana Rais Samia kwa namna alivyosimamia zoezi hili, tuna imani naye katika uboreshwaji mazingira rafiki ya biashara kwa wamachinga”
Naye, Mbunge wa Mbeya Mjini Dkt.Tulia Ackson, ameiomba Serikali kuharakisha mchakato wa Ujenzi wa barabara ya njia nne kuanzia eneo la Mlima Nyoka, Uyole hadi Mwanjelwa, ili kuondoa changamoto ya foleni katika barabara hiyo muhimu katika sekta ya usafirishaji.
Akijibu maombi ya Mbunge wa Mbeya Mjini, Waziri Mkuu amewahakikishia wakazi wa Mbeya kuwa serikali iko katika hatua za awali za kukamilisha utaratibu wa ujenzi wa barabara hiyo, na pia amewasihi viongozi wa Mkoa wa Mbeya kuweka mikakati mizuri ya kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kupata fursa za kifedha kutoka katika asilimia kumi ya fedha za Halmashauri ili kuwawezesha kukuza biashara zao.
Akifanya ukaguzi wa ujenzi wa madarasa manane katika Shule ya Sekondari ya Mwashiwawala, ambayo yanajengwa kwa fedha za Uviko 19, Waziri Mkuu ameupongeza Uongozi wa Mkoa wa Mbeya kwa kusimamia vyema miradi yote ambayo inajengwa kwa fedha za serikali hususan miradi ya Uviko 19 ambayo tayari Mkoa huo umeanza ujenzi na uko katika hatua za mwisho za ukamilishaji wake.
Akizngumza baada ya kutembelea kiwanda cha East African Starch Limited, kinachochakata na kuliongezea thamani zao la mahindi kwa kuzalisha bidhaa mbalimbali kama vile wanga, glucose, mafuta ya kupikia ya mahindi (Corn Oil) na Chakula cha Mifugo, Waziri Mkuu amemuhakikishia muwekezaji huyo kuwa Serikali itaendelea kumlinda na kuhakikisha anapata mafanikio katika uwekezaji wake.
“Serikali itaendelea kufuatilia kila hatua ya uwekezaji katika kiwanda hiki na mkandarasi aliyetaka kuhujumu ujenzi huu Serikali itaendelea kumfuatilia na kuhakikisha ujenzi wa kiwanda hiki unakamilia”.
Waziri Mkuu alihitimisha kwa kuushukuru na kuupongeza uongozi wa Mkoa wa Mbeya kwa usimamizu mzuri wa miradi yote ya Serikali, kujenga mahusiano mazuri kati ya viongozi wa serikali wabunge, wawekezaji na wananchi pamoja na utekelezaji wa miradi wenye viwango na ubora. Waziri Mkuu amemaliza ziara yake ya kikazi mkoani Mbeya ambayo ililenga kukagua miradi ya maendeleo na utekelezaji wa miradi ya kijamii.
No comments:
Post a Comment