Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima amesema atawawajibisha Wakurugenzi wa Halmashauri mkoani hapa ambao katika maeneo yao kuna shule za kidato cha tano na sita zenye Mkondo wa Sayansi na hazina maabara.
Malima amesema hayo leo katika Shule ya Sekondari Handeni, akiwa kwenye ziara yake ya kutembelea Miradi ya Fedha za Mihamala ya Tozo za Simu na Uviko 19, zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Shule hiyo iliyopo katika Halmashauri ya Handeni Mji, ujenzi wake madarasa mawili na ofisi ya walimu umekamilika kwa asilimia 85 ambapo umegharimu Sh milioni 40.
"Tunamuandaa mtoto akawe injinia au daktari lakinj hatuna maabara, hii haina maana yoyote. Wakurugenzi na Maofisa Elimu mliangalie hili la nitawawajibisha.
"Idara ya Mkoa mpitie shule zote ambazo hazina maabara mtenge fedha mjenge maabara inayofanana na hawa watoto vinginevyo hawa hawaendi kuwa madaktari.
Sisi tunahangaika kwa ajili yenu fikirieni huko mbele muwe mainjinia, madaktari bila maabara haitawezekana.
"Watoto wote wana haki ya kupata elimu, ndiyo maana rais wetu Mama Samia anamwaga fedha kwa ajili hiyo. Ofisa Elimu kaa na wenzako muangalie namna Tanga itakavyozalisha mainjinia na wanataaluma wa uhakika," amesema Malima.
Aidha, Malima amesema amefuta uhamisho wa walimu wanaotaka kuhama kutoka Handeni kwenda Tanga Mjini.
"Walimu wa hapa wanapenda kuhama, nimefuta uhamisho wa walimu kutoka Handeni kwenda Tanga Mjini mbaki hapa mfundishe watoto wetu," amesema.
No comments:
Post a Comment