HABARI MSETO (HEADER)


December 07, 2021

Tanzania yaendelea kukataa mapendekezo hali ya haki za binaadamu


 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju akifungua mkutano huo.

 

Mtaribu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binaadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa.



Baadhi ya wadau walioshiriki mkutano huo kutoka taasisi mbalimbali.


Na Irene Mark

LICHA ya takwimu kuonesha kwamba kiwango cha Tanzania kukubali mapendekezo yanayotolewa na nchi wanachama juu ya sheria mbalimbali zinazokiuka haki za binadamu kinazidi kushuka, serikali imesema maoni yote yaliyowasilishwa kwao yatafanyiwa kazi kwa mujibu Katiba, Sera, Mila na Desturi.

Kauli ya serikali imetolewa Dar es Salaam leo Desemba 7,2021 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju alipokuwa akifungua kikao cha kujadili ripoti ya tatu ya mapitio ya hali ya Haki za Binadamu (UPR) kwa  mwaka 2021, kilichoandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kwa kushirikiana na Kituo cha Msaada wa Sheria na  Haki za Binadamu (LHRC) na Shirika la Save the Children.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na THRDC, kiwango cha kukubalika kwa mapendekezo yanayotolewa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa juu ya sheria mbalimbali zinazokiuka haki za binadamu, unazidi kupungua kutoka asilimia 70 mwaka 2011 hadi asilimia 58 mwaka 2016 mpaka asilimia 43 mwaka huu 2021.

Mtandao huo umebainisha kwamba mwaka huu, Tanzania imefanya mapitio ya tatu ya hali ya haki za binadamu, ambapo ilipokea jumla ya mapendekezo 252 kutoka nchi mbalimbali, kati yake ni mapendekezo 108 sawa na asilimia 43 yamepokelewa, mengine 12 sawa na asilimia 4.8 yakiahidiwa kuzingatiwa na mapendekezo 132 sawa na 52 hayakukubaliwaa.

Mpanju amesema serikali haiwezi kupokea mapendekezo bila kuyasoma kwa umakini ili kuepuka kuruhusu masuala ya ushoga yanayokwenda kinyume na taratibu zote za nchi yetu.

“Tukiwa kule Geneva wakati wa kuyapitia mapendekezo haya tunakuwa makini mno maana kuna yale maneno madogo yapo mwisho kabisa sasa tukikubali kila kitu tutajikuta tunakubali ushoga na usagaji mambo yanayokwenda kinyume na sheria za nchi, mila, desturi hata vitabu vya Mungu vinakataa,” amesema Mpanju.

Hata hivyo ameupongeza Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu na Asasi zite za Kiraia, kwa kuwa karibu na serikali na kutoa mchango mkubwa katika upatikanaji wa haki kwa makundi yote ya binadamu nchini.

“Asasi za Kiraia ni mkono wa kuume wa Serikali, maana zinafika hata tusikofika hivyo kutusaidia kwa kiasi kikubwa kuyafahamu mahitaji ya watu, katika eneo hili la haki za binadamu,” amesema Mpanju.

Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa, amesema Mtandao huo unaratibu, kufuatilia na kufanyia tathmini ya Mapitio ya Hali ya Haki za Binadamu (UPR) kwa niaba ya Watetezi wa haki za binadamu ambao ni zaidi ya 200 hapa nchini.
 
“Mchakato huu unaendeshwa na serikali wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhakiki hali ya Haki za Binadamu ili kuboresha hali ya Haki za Binadamu katika nchi zote wanachama na kushughulikia ukiukaji wa haki za binadamu ili kuifanya dunia kuwa sehemu salama kwa kila binadamu,” amesema Olengurumwa.

No comments:

Post a Comment

Pages