HABARI MSETO (HEADER)


December 07, 2021

KAMISHNA WA MADINI ASHIRIKI KONGAMANO LA KIMATAIFA ZANZIBAR


Kamishna wa Madini kutoka Wizara ya Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga leo ameshiriki Kongamano la Kimataifa lililofanyika Zanzibar ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara lililokutanisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi ikiwa ni pamoja na Misri na China.

Katika kongamano hilo watendaji wa Taasisi zilizopo chini ya Wizara walioshiriki ni pamoja na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Dkt. Mussa Budeba, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Mratibu wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), Daniel Kidesheni na wataalam kutoka Wizara na Taasisi zake.

Akizungumzia ushiriki wa Wizara kwenye kongamano hilo, Dkt. Mwanga amesema kuwa lengo  ni kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo katika Sekta ya Madini na kubadilishana uzoefu na washiriki wengine wa kongamano hilo.

"Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Madini imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha Sekta ya Madini inakua kwa kasi, na moja ya mikakati ni pamoja na kutangaza fursa za uwekezaji kupitia makongamano na maonesho ya kimataifa," amesema Dkt. Mwanga.

Katika hatua nyingine, ametumia fursa hiyo kuwaalika wananchi wengi kujitokeza kuwekeza kwenye Sekta ya Madini.

Awali akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi amesema kuwa Serikali zote mbili zimeweka mazingiza mazuri ya uwekezaji na kuwaalika wawekezaji kujitokeza kwa wingi kuwekeza kwenye sekta mbalimbali.

Ameongeza kuwa, waasisi wa Tanzania wameweka misingi mizuri ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na sera na sheria bora ambapo zimeendelea kuboreshwa ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi.

No comments:

Post a Comment

Pages