· Rais Samia apongeza mpango wa NTDs kwa kazi nzuri
· Dk. Mollel ataka kasi zaidi kuyatokomeza
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imesema inaweka mipango sawa ili kuhakikisha angalau wagonjwa 60 wa mabusha wanafanyiwa kwa siku ili kupunguza idadi ya watu wenye ugonjwa huo nchini.
Ahadi hiyo ilitolewa siku ya Jumapili na Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kama mabusha na matende, kichocho, usubi, na trakoma
Alisema kwa kuwa serikali imeziwezesha hospitali zote za mikoa kambi maalum zinaweza kuandaliwa kwaajili ya kupeleka watalamu kwenye maeneo ya tatizo hilo ili kuharakisha upasuaji kwa watu wenye shida ya mabusha ambao wanakadiriwa kufikia 29,500.
Alisema kasi ambayo mpango wa taifa wa kudhibiti magonjwa hayo inaenda nayo ni ndogo na iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa inaweza kuchukua miaka mingi kuwafikia wananchi wenye shida hiyo kwa kuwa takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa ni watu 8,191 tu waliofanyiwa upasuaji mpaka kufikia mwaka jana.
“Sijaagiza mkafanye hivyo ila nijambo ambalo tukijipanga linatekelezeka. Njooni ofisini kwangu tukae tujone kana inawezekana tufanye hivyo namimi naamini kabisa inawezekana kwasababu kumfanyia upasuaji mgonjwa wa mabusha hakuhitaji ubobezi saana” alisema Dk. Mollel
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo kwa mwaka watu wasiozidi 1,200 ndio wamekuwa wakifanyiwa upasuaji wa mabusha kwa mwaka ambao ni wastani wa watu wanne kwa siku kasi ambayo Waziri alishauri iongezwe mpaka kufikia upasuaji wa watu 60 kwa siku.
“Mh Rais anatambua kazi yenu na anawapongeza sana mmefanyakazi kubwa sana kwasababu mlianza kuyapunguza kwenye wilaya 119 na sasa zimebaki wilaya tisa haya ni mafanikio makubwa sana na mnahitaji pongezi na serikali itakaa nanyinyi tuone namna ya kwenda kasi zaidi,” alisema
Meneja Mpango huo, Dk. George Kabona alisema kwa sasa gharama ya upasuaji wa mabusha kwa mtu mmoja inakadiriwa kufikia Sh 250,000 na mpaka kufikia mwaka 2021 mpango huo umeshawafanyia upasuaji watu 8,191 na nchi nzima inakadiriwa kuwa na wagonjwa 29,500 wenye mabusha.
Alisema mwaka 2008, mpango huo ulifanikiwa kuwafanyia upasuaji wagonjwa 200, mwaka 2013 wagonjwa 680, mwaka 2015 wagonjwa 315, mwaka 2016 wagonjwa 709 na mwaka 2017 wagonjwa 1,239 wakati mwaka 2018 walifanyiwa wagonjwa 1,441.
Dk. Kabona alisema mwaka 2019 mpango huo ulifanikiwa kuwafanyia upasuaji watu 1,387, mwaka 2020 watu 1,054 wakati mwaka 2021 walifanya upasuaji kwa watu 1,116 na kwamba mpango huo ulizinduliwa mwaka 2009 kwa ushirikiano na Shirika la Kudhibiti Usubi Afrika na Shirika la Misaada la Marekani USAID.
No comments:
Post a Comment