Mmoja wa Wakuu wa Shule katika Manispaa ya Moshi akipokea Kompyuta kutoka kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda wakati wa uzinduzi wa Mradi wa TEHAMA kwa Shule za Sekondari za Serikali.
Na WyEST, Kilimanjaro
Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda amesema Serikali
itahakikisha inaweka mgawanyo sawa wa rasilimali za elimu nchi nzima ili
kuwezesha watoto wote wa Kitanzania kupata elimu na mazingira bora ya
ujifunzaji.
Akizungumza
katika uzinduzi wa Mradi wa TEHAMA kwa Shule za Sekondari za Serikali
uliofanyika katika Shule ya Sekondari Mawenzi Mjini Moshi Waziri huyo
amesema kuwa ni lazima watoto wote wa Kitanzania wapate fursa sawa
kwenye elimu bila kujali eneo analotoka.
"Mgawanyo
wa fursa za elimu nchi nzima ni lazima uwe sawa na wa haki ili mtoto
asije kukosa fursa nzuri kwa sababu amezaliwa katika Wilaya fulani na
mwingine wa Wilaya nyingine anapata fursa nzuri zaidi wakati watoto wote
hawa ni Watanzania," amesema Prof. Mkenda.
Profesa
Mkenda amesisitiza kuwa Serikali inataka kuona TEHAMA inatumika katika
kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu pamoja na kuimarisha ubora wa
mafunzo.
Waziri Mkenda
amesema kuwa katika kufanikisha hilo Serikali imeendelea kuweka
msisitizo katika maeneo ya Sayansi na Teknolojia ili kuwezesha
Watanzania kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia ikiwa ni pamoja na
kuandaa mitaala ya elimu, miongozo na kutunga Sera zinazohusu matumizi
ya TEHAMA na Teknolojia saidizi.
Mhe.
Mkenda ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuwajengea uwezo walimu wa
Msingi, Sekondari na Wakufunzi wa Vyuo vya Ualimu kuhusu matumizi ya
TEHAMA kama nyenzo ya kufundishia na kujifunzia, ambapo mpaka kufikia
mwaka 2021 zaidi ya walimu 1,693 walipatiwa mafunzo ambapo kati yao
wakufunzi na walimu wa Sekondari na Msingi wenye mahitaji maalum ni 350.
Prof.
Mkenda amesisitiza kuwa kupitia Mradi wa Secondary Education Quality
Improvement Program (SEQUIP) itawezesha kuandaa Mkakati wa TEHAMA wa
elimu ya Sekondari ambao utanufaisha makundi yote ikiwa ni pamoja na
walimu na wanafunzi wenye mahitaji maalum katika shule 1,500 za Serikali
pamoja na kuandaa moduli na miongozo ya kufundishia TEHAMA kwa walimu
kazini wa shule za Sekondari.
Naye
Mkurugenzi wa Shirika la African Child, Catherine Kimambo amesema Mradi
wa TEHAMA kwa Shule za Sekondari za Serikali ni muhimu kwa kuwa
unajielekeza kusaidia kuongeza fursa ya upatikanaji wa elimu nchini.
Kimambo
amesema kuwa mradi huo ambao ni ushirikiano wa taasisi yake, Vodacom
Tanzania na Taasisi ya Teknolojia Dare es Salaam (DIT) utawafikia
wanafunzi 43, 291 katika shule 50 kutoka katika mikoa 10 ukilenga kutoa
mafunzo kwa walimu 100 wa TEHAMA, kugawa kompyuta 186, vishikwambi 246,
kadi za simu zenye gb 50 kila mwezi kwa kipindi cha mwaka mmoja kutoka
Vodacom Tanzania.Aidha watatoa mafunzo ya awali ya kidijitali kupitia
wanafunzi wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Vodacom Tanzania Stholizwe Mdlalose amesema wamejiunga
katika mradi huo kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora na
kuongeza fursa za elimu kwa wote huku akijivunia ushiriki wa Vodacom
katika kusaidia maeneo mbalimbali ya sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na
kutoa huduma ya mtandao kwa shule, vifaa vya kufundishia na kujifunzia
zikiwemo kompyuta na uwepo wa mfumo wa ujifunzaji E- Fahamu.
Stholizwe
amesisitiza kuwa Kupitia Vodacom Foundation, zaidi ya shule 450 nchini
wanapata fursa za kujifunza kupitia mtandao ambapo mafanikio hayo
yametokana na ushirikiano wa wadau mbalimbali ikiwemo Mfuko wa
Upatikanaji wa Huduma za Mawasiliano ya Universal (UCSAF), ambapo mwaka
jana walitoa kompyuta, 1,400, na mtandao wa intaneti ulionganishwa kwa
shule za msingi na sekondari katika maeneo mbalimbali ya nchi ambayo
yamekuwa hayana huduma hiyo.
No comments:
Post a Comment