Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wametembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa lengo la kuhamasisha utalii wa ndani pamoja na kuadhimisha miaka 45 ya Chama cha Mapinduzi.
Akizungumza katika ziara hiyo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amewapongeza UWT Taifa kwa kufanya ziara hiyo.
“Kwa hiki kitendo mlichokifanya mmekuwa mabalozi wakubwa ambao tunategemea mtaleta makundi mengine kutembelea hifadhi zetu na maeneo mengine yaliyo na vivutio Tanzania nzima ” Mhe. Masanja amesema.
Amefafanua kuwa kupitia utalii wa ndani Tanzania inatangazwa ndani na nje ya nchi lakini pia watalii wanachangia katika pato la Taifa.
Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mstari wa mbele kutangaza utalii.
“Kipekee namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kiungo katika kuhamasisha Utalii wa ndani lakini pia naushukuru uongozi wa UWT Taifa na washiriki wote kwa kumuunga mkono Mhe. Rais kuja kutembelea Hifadhi yetu ya Serengeti.”
Katika kuendeleza kutangaza utalii wa ndani, Mhe. Masanja amesema kuelekea Maadhimisho ya Siku ya wanawake duniani atahamasisha wanawake nchi nzima kutembelea kivutio cha utalii kilicho katika maeneo wanayoishi ili kutangaza utalii wa ndani.
Naye, Mwenyekiti wa UWT Taifa, Gaudensia Kabaka ameahidi kwamba UWT itakuwa balozi katika kutangaza utalii.
“Sisi tutakuwa mabalozi wa utalii wa ndani tukimuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na kwamba furaha yake ni kuona kwamba wanahamasisha utalii wa ndani kupitia wanawake zaidi ya 100 waliotoka katika mikoa yote nchini Tanzania.
Amesema watahamasisha makundi mengine kutembelea mbuga za wanyama ili kuchangia pato la Taifa.
Ameongeza kuwa Watanzania wabadili fikra za kuona kwamba wazungu ndio wanaoweza kuingiza fedha katika Sekta ya Utalii na badala yake wabadilike kwa kuwa wazalendo kutembelea vivutio vya utalii ili kuchangia pato la Taifa.
Katika hatua nyingine, katika ziara hiyo umezinduliwa utalii wa michezo ambao pamoja na mambo mengine watalii watakaotembelea hifadhini watapata fursa ya kushiriki katika michezo mbalimbali kama kuvuta kamba, netball, kukimbia na magunia n.k.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) (kushoto) akimkabidhi zawadi ya kalenda Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania, Gaudensia Kabaka wakati wa ziara ya UWT Taifa kwenye Hifadhi ya Taifa ya Serengeti .
No comments:
Post a Comment