HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 28, 2022

WAKAZI Kiwangwa walia na wizi wa mifugo, waitaka serikali ichukue hatua

 



Na Julieth Mkireri, KIWANGWA


BAADHI ya Wakazi wa Kijiji cha Msinune Kata ya Kiwangwa Wilaya ya Bagamoyo wamelaani vitendo vya wizi wa mifugo vinavyotokea mara kwa mara  huku wakiomba Serikali kuchukua hatua zaidi kuvikomesha.


Wakizungumza kwa njia ya simu kwa nyakati tofauti wahanga wa matukio hayo walisema wanaohusika na matukio hayo wamekuwa wakitoroka baada ya mifugo kupatikana huku wanaohisiwa wakiendelea kuachwa mtaani.


Mmoja wa wahanga wa tukio la wizi lililotokea usiku wa kuamkia Februari 26 Benard Kutu amesema alipigiwa simu usiku na kijana anayesimamia mifugo yake huko katika kijiji cha Msinune akielezwa kuhusiana natukio na ng'ombe wake nane kuibiwa.


Kutu amesema baada ya kupokea simu hiyo alimuelekeza kijana wake kutoa taarifa kwa viongozi wa Kijiji  mwenyekiti na mtendaji na polisi ili hatua za kuwasaka wezi zifanyike haraka.


"Baada ya kupokea simu usiku wa saa kumi kama na dk 20 hivi kijana wangu aliniambia amekuta walinzi wamefungiwa ndani huku zizi likiwa jeupe ng'ombe wote wakiwa wameibiwa na watu wasiojulikana nilimjulisha kaka yangu na mdogo wangu ili waende kunisaidia kuwasaka" alisema.


Amesema msako uliofanyika ulifanikisha ng'ombe wake kupatikana porini lakini wezi hawakukamatwa kwani walifanikiwa kukimbia.


Mlinzi wa mifugo ya Benard, Ismail Chanzenze alieleza kuwa majira ya saa tisa usiku alisikia mbwa wanabweka na alipotoka nje alimulikwa na tochi na alifanikiwa kuwaona watu wawili jamii ya wamasai.


Amesema baada ya kuona hali hiyo aliingia ndani kumuamsha mlinzi mwenzake aliyekuwa amelala, lakini  wakati akikimbilia ndani aliwaonda watu wawili wakiwa wanapiga taa kuzivunja na wengine watatu wanazunguka kwenye zizi la Ng'ombe.


Ismail amesema, alipoingia ndani wale watu waliendelea  kupiga taa wakitumia fimbo zao huku wakiwatishia kutulia ndani na atakayethubutu kutoka watamchoma mshale.


"Tukiwa ndani na mwenzangu tuliendelea kupiga kelele za kuomba msaasa lakini hakuna aliyetokea huku wale watu walioko nje waliendelea kutukalipia tutulie tukiendelea na kelele zetu watavunja mlango" amesema.


Hata hivyo amebainisha kuwa baada ya muda mfupi msimamizi wao anayejulikana kwa jina la Kimungu Rajabu alifika na kuwauliza sababu za kelele walizokuwa wanapiga .


Rajabu ambaye alikuta walinzi hao wakiwa wamefungiwa kwa nje aliwafungulia mlango na walipotoka kukagua nje walikuta mifugo yote imeibiwa na wezi wametokomea nayo.


Amesema walitoa taarifa kwa mmiliki wa mifugo na viongozi wengine wa kijiji  na polisi ambao walifika na walinzi hao kuwekwa chini ya ulinzi hadi baadae walipotolewa kwa dhamana baada ya mifugo kupatikana.


Mtendaji wa Kata ya Kiwangwa Sada Madie amekiri kuwepo kwa matukio ya wizi katika eneo lake huku akisema hajapata taarifa ya tukio la Kijiji cha Msinune. 


"Wizi wa mifugo kwenye kata yangu ni ugonjwa mkubwa tu na wanaotuhumiwa mara nyingi ni hawa wafugaji jamii ya wamang'ati ambao sio wakazi wa hapa wanakula njama na watu wa karibu wanaoibiwa mifugo" amesema Sada.


Mwenyekiti huyo wa kamati ya ulinzi na Usalama kata ya Kiwangwa alisema wamekuwa wakifanya vikao vya mara kwa mara na wananchi kuhusiana na suala hilo lakini wapo watu wanatajwa kuhusika kula njama na wezi na watu hao wamekuwa wakionekana kwa msimu kwenye kata hiyo.


Sada amesema jitihada za kuwasaka wanaotuhumiwa zinaendelea ili wafikishwe kwenye mikono ya sheria.


Diwani wa Kiwangwa Malota Kwaga amekiri kupata taarifa za mwananchi wake wa Msinune kuibiwa mifugo ambapo aliwaonya wananchi kuachana na tabia hiyo huku akiwaasa kutoa ushirikiano kuwapata wahusika na kuepuka kujichukulia sheria mkononi.


Victor Shemtawa ambaye alishiriki kusaka mifugo hiyo hadi kupatikana aliwashauri wananchi kujenga tabia ya ulinzi shirikishi na kila mmoja kuwa mlinzi wa mwingine ili kuwafichua wezi na kutokomeza tabia hiyo kwa jamii.


Mwenyekiti wa kijiji cha Msinune Nyemo Sahali amesema wananchi wamechoshwa na matukio hayo ambayo yanawarudisha nyuma na kwamba wanatarajia kufanya mkutano wa kuweka mikakati ya namna ya kukomesha matukio hayo.


Amesema katika kipindi cha mwezi Januari na Februari  mwaka huu tayari matukio mawili yametokea likiwemo la wizi wa mbuzi 15 ambazo hadi leo hazijapatikana.


No comments:

Post a Comment

Pages