HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 13, 2024

Rais Mwinyi afungua Onesho la 8 Swahili International Tourism Expo

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametoa pongezi kwa juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuimarisha sekta ya utalii nchini. Alisisitiza kwamba idadi ya watalii wa kimataifa wanaotembelea Tanzania imeongezeka kwa kasi, sambamba na ongezeko la mapato kutoka sekta hiyo.

Katika hotuba yake iliyotolewa wakati wa ufunguzi wa Onesho la 8 la Utalii la Kimataifa la Swahili (S!TE 2024) , katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, Dkt. Mwinyi alieleza kuwa sekta ya utalii imekuwa nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa nchi. Alitaja takwimu za hivi karibuni zikionyesha kuwa, hadi kufikia mwezi Agosti 2024, Tanzania ilikuwa imepokea watalii 2,026,378, ikiwa ni idadi ya juu kabisa kuwahi kufikiwa katika historia ya nchi.

Dkt. Mwinyi amebainisha  kuwa mapato yatokanayo na sekta ya utalii yamefikia Dola za Marekani bilioni 3.5, na sekta hiyo inachangia asilimia 17.2 ya Pato Ghafi la Taifa na asilimia 25 ya mauzo ya nje. Aidha, sekta ya utalii inatoa ajira zaidi ya milioni 1.5, ikijumuisha ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.

 Amesisistiza kuwa  mafanikio hayo yamewezesha Tanzania kutambuliwa kimataifa, na kwamba nchi hiyo imeshinda tuzo mbalimbali. Taarifa kutoka Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism – World Tourism Barometer) inaonyesha kuwa Tanzania inashika nafasi ya 6 duniani na ya kwanza barani Afrika kwa kuwa na ongezeko kubwa la watalii.

Miongoni mwa tuzo zilizotajwa na Dkt. Mwinyi ni zile zilizotolewa mwaka 2023 na World Travel Awards (WTA), ambapo Bodi ya Utalii Tanzania ilitambuliwa kama "Africa’s Leading Tourist Board," Kisiwa cha Thanda Shunghumbili, Mafia kilitambuliwa kama "World Leading Exclusive Private Island," na Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kama "Africa’s Leading Tourist Attraction."

Kwa ujumla, Dkt. Mwinyi  ameridhishwa na hatua zinazochukuliwa na serikali katika kukuza utalii, akiongeza matumaini ya kuendelea kwa maendeleo katika sekta hii muhimu kwa uchumi wa nchi.



No comments:

Post a Comment

Pages