Na Jasmine Shamwepu, DODOMA
KATA ya Msalato katika Jiji la Dodoma inakabiliwa na kero ya kukosekana kwa maeneo kwa ajili ya ujenzi wa huduma za kijamii ikiwemo eneo la makaburi hali inayosababisha watu kuzikana kwenye maeneo ya makazi.
Diwani wa kati hiyo Nsudi Bukuku, alibainisha hayo jana alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha kutatua mgogo wa ardhi baina ya Jeshi la Magereza na wakazi wa kata ya Masalato, Makutupola pamoja na Mbalawala kilicho andaliwa na mkuu wa mkoa Antony Mtaka.
Bukuku, alisema hali hiyo inatokana na Kata hiyo kuzungukwa na taasisi za serikali ikiwemo Jeshi la Magereza, Jeshi la Wananchi (JWTZ) na mradi wa ujenzi wa kiwanja cha ndege cha kisasa Msalato.
Alkisema kutokana na hali hiyo maeneo kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya huduma za kijamii kama shule na vituo vya afya yamekosekana.
“Ndugu mkuu wa mkoa sisi hapa Msalato tuna kero kubwa sana ya maeneo kwa ajili ya ujenzi wa huduma za kijamii kama vile shule, kituo cha afya pamoja na maeneo kwa ajili ya kuzikana hali inayotulazimu kuzikana kwenye maeneo ya makazi yetu”alisisitiza Bukuku
Aidha, alisema hivi sasa shule ya msingi ambayo walikuwa wakitegemea eneo lake limechukuliwa na mradi wa ujenzi wa kiwanja cha ndege cha kisasa.
“Shule ya msingi ambayo tulikuwa tukitegemea kwa miaka mingi watoto wetu wasome emechukuliwa na mradi wa ujenzi wa uwanja wa ndege hivyo hivi sasa tunasubiri notis ya kuondolewa na mpaka sasa hatuna eneo ambalo tunaweza kwenda kujenga shule nyingine hivyo mkuu wa mkoa tunaomba tupatiwe eneo”alisisitiza Bukuku
Alisema, maeneo ambayo walikuwa wanayetegemea kujenga huduma za elimu na afya kwa asilimia kubwa yanamilikiwa na Jeshi la Magereza na Jeshi la wananchi (JWTZ) Msalato.
“Haya maeneo ya karibu yote yamechukuliwa na taasisi hizi mbili pamoja na uwanja wa ndege na eneo ambalo wanatupa kwenda kujenga ni mbali takribani kilomita 15”alisema
Naibu waziri wa kilimo na mbunge wa jimbo la Dodoma Antony Mavunde, alisema ukosefu wa maeneo kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maendeleo katika kata hiyo imekuwa kero kwa wananchi.
“Eneo la Msalato ni Kata ambayo imebahatika kuwa na miradi mikubwa ya kimaendeleo lakini hivi sasa kumekuwepo na changamoto ya ukosefu wa maeneo kwa ajili ya ujenzi wa huduma za kijamii kama vile shule na vituo vya afya na hata maeneo ya maziko”alisema
Alisema serikali imetoa kiasi cha Sh.milioni 450 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya msingi lakini eneo walilopatiwa kwa ajili ya kujenga shule hiyo itawalazimu wanafunzi kutembea umbali kilomita 15 kila siku kinyume na sera ya elimu inayotaka huduma kama hizo kuwa eneo la karibu na jamii.
Mkuu wa mkoa alisema amepokea malalamiko ya pande zote na atakwenda kuyawasirisha katika mamlaka zinazo husika ili kupata majibu ya kero zote katika kata hizo tatu.
No comments:
Post a Comment