Mwenyekiti wa TAPSEA, Zuhura Songambele akizungumza na waandishi wa
habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu mkutano wao mkuu utakaofanyika
mkoani Dodoma, kuanzia Mei 31 hadi Juni 4 mwaka huu.
Na Mwandishi Wetu
RAIS
Samia Suluhu Hassan, anaratajiwa kufungua Mkutano Mkuu wa Chama cha
Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) utakaofanyika mkoani Dodoma kuanzia
Mei 31 hadi Juni 3 mwaka huu.
Hayo
yamesemwa na Mwenyekiti wa TAPSEA, Zuhura Songambele wakati akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, ambapo amesema pamoja
na mkutano pia kutakuwa na uchaguzi mkuu Juni 3,2022.
Amesema mkutano huo mkuu unatarajiwa kukutanisha makatibu muhtasi na wadau wengine 4,000 kutoka kila kona ya nchi.
"TAPSEA
ina wanachama 3,413 tunaamini watashiriki wote, ila kwa ujumla mkutano
unaweza kukutanisha washiriki 4,000," amesema mwenyekiti.
Songambele
amesema kuanzia Mei 31 na Juni mosi wanachama wa TAPSEA watapata fursa
ya kujifunza mambo mbalimbali kuhusu sekta hiyo, hivyo kuwataka
washiriki kwa wingi.
Amesema wamealika watoa mada mbalimbali ambao watatumia mkutano huo kuwapiga msasa wanachama wao.
"Tunapenda
kutumia nafasi hii kuwakaribisha wana TAPSEA wote katika mkutano wetu
unaotarajiwa kufunguliwa na Rais Samia. Nadhani wanaelewa kuwa jambo la
mama ni jambo letu. Tuje kwa wingi kumsikiliza mama yetu naamini atajibu
baadhi ya changamoto tunazopitia,"amesema.
Amesema
Juni 3,2022 itakuwa siku ya mkutano mkuu na uchaguzi hivyo wana TAPSEA
wote wanaruhusiwa kugombea, ili kupata viongozi wanawataka.
Songambele
amesema katika uchaguzi huo nafasi zinazogombewa ni Mwenyekiti, Makamu
Mwenyekiti, Katibu, Naibu Katibu, Mwekahazina na Wajumbe tisa.
Aidha,
alitoa rai kwa viongozi wa Serikali na taasisi za umma kutoa ruhusa kwa
makatibu muhtasi hao ili waweze kushiriki mkutano muhimu kwao.
Kwa upande mwingine Songambele amesema zipo baadhi ya changamoto wanakutana nazo ila wamekuwa wakizipatia ufumbuzi kwa wakati.
No comments:
Post a Comment